Latest Posts

MZEE BUTIKU AOMBA RAIS SAMIA AUNGWE MKONO KUPAMBANA NA UTEKAJI NA MAUAJI

Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Mzee Joseph Butiku, ameonesha masikitiko yake juu ya matukio ya utekaji, mauaji, na vitendo vingine vya uhalifu vilivyoongezeka nchini, huku akiomba Watanzania wote kushirikiana na serikali katika kupambana na wahalifu.

Akizungumza mbele ya wanahabari Septemba 10, 2024 jijini Dar es Salaam, Mzee Butiku amesema kuwa wahalifu hao wanaishi miongoni mwa raia na kuwa ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia vyombo vya dola ili hatua zichukuliwe.

“Sisi Watanzania ni wastaarabu, tusiseme hatuwajui wahalifu hawa, ukweli ni kwamba tunawajua, wanaishi miongoni mwetu na katika kaya zetu, wapo ndani ya vyombo vyetu vya dola. Hapa ni lazima serikali yetu iwajue,” amesema Mzee Butiku.

Mzee Butiku amesisitiza kuwa, licha ya changamoto hizo, vyombo vya dola nchini vina uwezo mkubwa wa kushughulikia vitendo vya uhalifu, lakini amehimiza kuwa taarifa sahihi lazima ziwe zinatolewa kwa Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kuchukua hatua stahiki.

“Nchi yetu imeviwezesha vyombo hivyo kuwa na uwezo wa kutosha wa utaalamu na uwezo wa vitendea kazi. Viongozi wa vyombo hivyo wasituambie kwamba hawajui kinachotokea, wanajua. Tumuunge mkono Rais wetu, tusiogope.” Amesisitiza Mzee Butiku.

Katika mazungumzo yake, Mzee Butiku alihimiza umuhimu wa Watanzania wote kufuata Katiba na sheria za nchi, akisisitiza kuwa utulivu na amani vinaweza kupatikana tu ikiwa kila raia atatii misingi ya kikatiba.

“Ninapenda kupendekeza kwa Watanzania wote kuamini na kukubali kuwa Taifa letu si la wauaji wala la wahuni, ni Taifa la watu wanaoishi katika kuzingatia Katiba ya nchi yetu na sheria zinazotokana na Katiba hiyo,” alisema na kuongeza,

“Tuna Rais mmoja tu, sio wawili wala watatu, tuliyemkabidhi Katiba ya nchi yetu ili aitumie kuongoza Taifa letu. Tumuunge mkono Rais wetu bila kusita katika kupambana na matukio ya utekaji, mauaji, ulawiti, na ubakaji.”

Tamko hili la Mzee Butiku limekuja wakati ambapo Taifa linaendelea kukumbwa na matukio ya kutatanisha, ikiwa ni pamoja na kifo cha kiongozi wa CHADEMA, Mzee Ali Mohamed Kibao, ambaye aliuawa baada ya kutekwa. Kifo chake kimesababisha wasiwasi mkubwa, huku wanasiasa, mabalozi, na mashirika ya haki za binadamu wakiendelea kutoa wito wa uchunguzi huru na uwajibikaji.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!