Na; Abdallah Khamis
Takribani siku 30 sasa zimepita tangu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa amueleza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa tukio la mgonjwa aliyeonekana kubebwa katika tenga kutoka katika kituo cha afya Mchoteka na kuhamishiwa katika Hospitali ya Misheni ya Mbesa, mkoani Ruvuma kuwa ni njama za kisiasa na kwamba hakuna tukio hilo au lolote linalofanania na hilo lililotokea katika mji wa Tunduru, mkoani humo, Jambo TV kupitia ufuatiliaji wake imebaini kuwa huenda viongozi hao (Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mohamed Mchengerwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan) walidanganywa na wasaidizi wao juu ya uhalisia wa tukio hilo
Kwa mujibu wa taarifa fiche na za kiuchunguzi ilizozipata Jambo TV kuanzia katiki vijiji vya Marumba, Mchoteka na Mbesa vilivyopo katika wilaya ya Tunduru, mkoa wa Ruvuma inadaiwa kuwa idadi ya wagonjwa waliobebwa kwenye tenga siku hiyo ilikuwa ni watatu (3) ambapo wagonjwa hao wametambuliwa kuwa ni Zainabu Ali Saidi, Ikram Mohamed Mbela (mtoto) na mwanaume mtu mzima ambaye jina lake halijapatikana mara moja, ambao wote hao siku ya tukio waliungua moto wakiwa ndani ya nyumba yao katika kijiji cha Marumba, Tunduru, na kwa sasa Zainab Ali Said na Ikram Mohamed Mbela wamefariki kwa nyakati tofauti wakiwa kwenye Hospitali ya Misheni Ndanda, iliyoko mkoani Mtwara walipohamishiwa kwa matibabu kutoka Mbesa
Inaelezwa kuwa kabla ya umauti wao Zainab na Ikram wakiwa wagonjwa walipokelewa katika Hospitali ya Misheni Ndanda Septemba 27.2024 majira ya saa 06:59 usiku na kuanza kupatiwa matibabu, lakini ilipofika alfajiri ndugu wa wagonjwa hao wakaelezwa uwepo wa msiba wa mgonjwa mmoja
Jambo TV imeelezwa kuwa mgonjwa aliyetangulia kufariki Dunia kutokana na ajali hiyo ya moto ni mtoto Ikram Mohamed Mbela mwenye umri wa miaka miwili (2) aliyefariki Septemba 27 mwaka huu (2024) ikiwa ni muda mfupi baada ya Waziri Mchengerwa kumtaarifu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na umma wa Watanzania kuwa hakuna tukio hilo la watu kubebwa katika tenga
Inaelezwa kuwa mtoto Ikram Mohamed Mbelwa amezikwa katika kijiji cha Mandia, kitongoji cha Miuru, wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara baada ya ndugu kueleza kuwa hawana uwezo wa kusafirisha mwili kwenda Tunduru
Aidha, Zainab Ali Said amefariki Dunia Oktoba 14.2024 katika Hospitali ya Misheni Ndanda alipokuwa akiendelea na matibabu
Ufuatiliaji wa Jambo TV umebaini uwepo wa jitihada kubwa za siri na zisizokuwa na dhamira njema za kufuta kumbukumbu zote za wagonjwa hao kutoka katika kituo cha afya Mchoteka kwa lengo la kuthibitisha kuwa wagonjwa hao hawajawahi kufikishwa katika kituo hicho
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Septemba 24 mwaka huu (2024) kwenye majira kati ya saa 4 hadi 5 usiku wakiwa katika kijiji cha Marumba Zainab na wenzake walipata ajali ya moto kwa nyumba yao kuungua wakiwa ndani na kuokolewa na majirani kisha kukimbizwa katika kituo cha afya Mchoteka
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Jambo TV Hamis Mohamed na Said Mabwila ambao ni madereva wa Bodaboda waliowabeba wagonjwa hao wameeleza kuwa shughuli hiyo ya kuwabeba wagonjwa kutoka kituo cha afya Mchoteka kwenda maeneo mengine ya matibabu inawaingizia kipato kati ya shilingi 20,000 hadi 25,000 kwa safari moja
Akisimuliza mkasa wa tukio hilo Hamis Mohamed amesema siku ya tukio walifanikiwa kuwaokoa majeruhi wa ajali ya moto wakiwa watatu (3) na kufanya jitihada za kuwasiliana na daktari aliye katika kijiji cha Marumba ambaye hakupatikana kwa wakati huo, kisha wakakata shauri kwenda kwenye Zahanati ya Mchoteka kwa kuwapakia wagonjwa hao kwenye Pikipiki mbili (2) tofauti
“Mmoja alikuwa ni mtoto tulipofika Hospitali tukapewa huduma ya kwanza vizuri tu wakatuambia wao hawana uwezo zaidi hivyo mgonjwa anapaswa kwenda Mbesa, ila gari hakuna, wakasema kama tutaweza kwenda na Pikipiki tuendelee nao kwa ajili ya kuokoa maisha yao maana hali yao ilikuwa mbaya sana” -Mohamed
Kwa upande wake, Mabwila amesema baada ya kufika Hospitalini hapo ilionekana wagonjwa hawawezi kutibiwa hivyo amedai kuwa walipewa dawa za kutuliza maaumivu pekee na kutakiwa kupelekwa Hospitali ya Misheni ya Mbesa, ambapo inadaiwa kuwa ubebaji huo wa wagonjwa umekuwa maarufu katika kata hiyo kutokana na kwamba wananchi wengi hushindwa kumudu gharama za kulipa kwenye gari maalum la kubeba wagonjwa pale wanapozidiwa
“Haya matenga tunakodi kwa mzee Simba (ni maarufu hapa kijijini) kwa kuwa anayatengeneza kwa ajili ya shughuli hiyo tu” -Mabwila
Ameeleza kuwa wakiwa katika kituo cha afya Mchoteka walishirikiana kwa karibu na daktari aliyemtaja kwa jina moja la Baraka na kwamba siku hiyo alilipwa jumla ya shilingi 25,000 kama dereva
“Nilimsafirisha mgonjwa kwa shilingi 25,000 na pale Mchoteka tulikuwa na Dkt. Baraka, nimeshapakia miili mingi mahututi kuikimbiza Hospital hiyo, lakini kuna changamoto kubwa sana unapopakia wagonjwa kwa mfumo huo, Pikipiki huwa inayumba sana kwa hiyo ni hatari kama sio dereva mzoefu unaweza kupata ajali” -Mabwila
Aidha, Mabwila ameongeza kuwa siku ya tukio hofu yake kubwa ilikuwa kukutana na mnyama Tembo njiani kwa kile alichoeleza kuaa safari za usiku ni hatari katika mazingira yao yenye wanyama wanaozurura hovyo,
Kama hiyo haitoshi, akizungumza na Jambo TV kwa njia ya simu Salum Simba (Mzee Simba) ambaye ni mtengeneza matenga katika kijiji cha Marumba wilaya Tunduru amesema kazi hiyo ya kutengeneza matenga kwa ajili ya kubebea wagonjwa ameifanya kwa zaidi ya miaka 10, na kwamba aliiona fursa hiyo baada ya kuwepo kwa changamoto ya kuwafikisha Hospitalini wagonjwa wasioweza kutembea
Amesema suala la wagonjwa kubebwa katika matenga linajulikana katika Zahanati ya Mchoteka na kunapokuwa na changamoto ya mgonjwa kusafirishwa hupatiwa taarifa za kukodisha tenga kwa wahusika
“Watu wengi ambao wagonjwa wao hawana uwezo wa kutembea labda ni mama mjamzito au mtu amevunjika mguu, madaktari wanawaelekeza waje kwangu kutafuta tenga, mimi ninakodisha tenga moja kwa shilingi 2,000 mpaka 3,000” -Mzee Simba
Kwa Upande wake, Mohamed Auni ambaye ni babu wa Ikram na mjomba wa Zainab (wale wagonjwa waliofia Hospitali) amesema usafiri wa gari la kuwasafirisha wagonjwa waliupata kutoka Hospitali ya Mbesa kwenda Ndanda, baada ya awali wagonjwa wake kufikishwa katika kituox cha Mbesa kutokea Mchoteka wakiwa katika matenga yaliyobebwa katika Pikipiki
“Nilimsikia Rais (Dkt. Samia Suluhu Hassan) na Waziri (Mohamed Mchengerwa) wanasema hili jambo si la kweli, mimi ndiye niliwauguza hawa wagonjwa katika hatua zote mpaka walipofariki kwa nyakati tofauti pale Ndanda Misheni , nimeshawazika mwanaangu na mjukuu wangu walioungua kwa moto na kubebwa katika Pikipiki kutokea kituo cha afya Mchoteka wakiwa wamewekwa kwenye tenga na kupakiwa kwenye Pikipiki” -Auni
“Nimesikitishwa na taarifa waliyompa Rais (Dkt. Samia Suluhu Hassan? kituo kile cha Mchoteka kinapokea wagonjwa wengi lakini hakina gari na wahusika wameficha udhaifu huu kwa ajili ya kulinda ajira zao na kumdanganya Rais nimeumia sana” -Auni
Katika mkakati wa kujiridhisha na madai hayo, mkazi mwingine wa kijiji hicho Ali Mtalika amesema ameshuhudia mara kadhaa wagonjwa wakibebwa katika matenga kwa usafiri wa Pikipiki kutokana na kukosa usafiri wa gari katika kituo cha afya Mchoteka
Mwanakijiji mwingine, Amina Mtenge naye ameungana na mtangulizi wake lakini analo la ziada kwamba njia ya kwenda Mbesa ina Tembo wengi hivyo kwa usafiri huo hasa nyakati za usiku siyo rafiki kabisa
Akizungumzia kadhia hiyo, Diwani wa kata ya Mchoteka Seif Dauda amesema ameshafanya jitihada kadhaa kuwaokoa wapiga kura wake ikiwamo kupeleka taarifa katika ngazi zote na kwamba hata ofisi zote za serikali Tunduru, zinajua kuhusu shida hiyo lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa japo shida hiyo ni ya muda mrefu, na kwamba haijaanza sasa
Amedai kuwa, jambo hilo sio geni na ni kitendo ambacho mpaka Bodaboda wamegeuza fursa kwa sababu wanasafirisha wagonjwa kila wakati
“Tunaomba mamlaka zione ili tupate gari, wajue walipakodi wa Tunduru tinapitia changamoto hizi, nimeshafika mpaka ofisi ya Mkuu wa mkoa (Ruvuma) lakini hakuna kilichofanyika” -Diwani
Inaelezwa kuwa, kituo cha afya Mchoteka licha ya kuanzishwa mwaka 1978 lakini hakina gari maalumu kwa ajili ya wagonjwa, mbinu ya kuwaweka wagonjwa katika tenga kisha kupelekwa na Bodaboda wanaopewa rufani ndiyo inayotumika hadi sasa
Akijibu madai hayo, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru Shija Marandu amekanusha vikali uwepo wa taarifa hizo kwa kueleza kuwa jambo hilo sio sahihi na kwamba anadai kuwa ‘limepikwa’ ili kukuza taarifa hizo za ‘uzushi’
Ameongeza kuwa gari la kubeba wagonjwa linakaa katika Hopsitali ya Misheni ya Mbesa iliyopo takribani kilometa 15 kutoka Mchoteka, na kwamba kunapotokea dharura madereva hupigiwa simu kwa ajili ya kubeba wagonjwa, hivyo hakukuwa na mgonjwa yeyote wa ajali ya moto aliyefikishwa katika kituo cha afya Mchoteka kama inavyoelezwa katika mitandao ya kijamii
Alipoulizwa kama taarifa iliyowasilishwa kwa Waziri Mchengerwa na baadayee kufikishwa kwa Rais Dkt. Samia ni sahihi Mkurugenzi huyo amejibu kuwa taarifa hiyo ni sahihi, na kwamba ndio maana imezungumzwa hata katika vyombo vya habari na Waziri mwenye dhamana ya OR-TAMISEMI
Akizungumzia juu ya kuijridhisha kwake kama siku ya tukio la mgonjwa anayedaiwa kubebwa katika tenga Marandu amesema aliomba taarifa kwa Mganga mkuu wa wilaya (DMO) na kwamba anaamini kuwa taarifa hizo alizopatiwa ni sahihi, na ndizo taarifa zilizowasilishwa kwa Waziri Mchengerwa na baadaye kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
Mkurugenzi huyo ameenda mbali zaidi kwa kusema kuwa, gari za kubeba wagonjwa (ambulance) zipo katika vijiji jirani na inapotokea mgonjwa mahututi anayehitajika kusafirishwa huwa wanazipigia simu zinakuja na kubeba wagonjwa
Amesema walipopata taarifa siku ya kwanza kuhusu madai hayo walituma watu kufuatilia na kwamba taarifa walizompa Waziri wa TAMISEMI ambaye baaye aliziwasilisha kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni sahihi, huku akitumia nafasi hiyo kuhoji sababu ya kutofikiwa kwa viongozi kwa ajili ya kutoa taarifa za kina
“Lakini pia tuna program ya M-mama inasaidia pale ambulance inapokuwa mbali na huwa wanatumia usafiri huo fedha inalipwa na serikali, hakuna kitu kama hicho mgonjwa asafirishwe kwenye tenga, mimi nimetoka hapo Hospital sijui hiyo picha wameitengezea wapi, hao ni watu wabaya sana” -Mkurugenzi
Kauli ya Mkurugenzi huyo inapingana kabisa na yale yaliyoelezwa na wakazi wa eneo hilo, Diwani, Bodaboda waliowabeba wagonjwa kutoka kwenye kituo cha afya na kuwafikisha kwenye Hospital ya Misheni Mbesa, na mashuhuda wengine
Kuhusu gharama kubwa ya usafiri wa gari, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Tunduru asema gharama ya usafiri huo inapangwa na wananchi wenyewe na kwamba hamna gharama kubwa na wala hawajashindwa kumpeleka mgonjwa anapopata rufani
“Na kwa wale wasio na uwezo huwa tunawabeba kwa gharama za Halmashauri tunapokuwa tumejiridhisha kwamba hali yao sio nzuri kiuchumi” -Mkurugenzi