Latest Posts

RC MALIMA AWATAKA MADIWANI KUKOMESHA HOJA ZA KUJITAKIA

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amewataka madiwani pamoja na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kuhakikisha wanakomesha hoja zinazotokana na uzembe na kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa majukumu yao ili kuondoa hoja za ukaguzi kwa wakati na kuharakisha maendeleo ya halmashauri hiyo.

Malima ametoa maelekezo hayo wakati akiongoza kikao maalumu cha Baraza la Madiwani cha kujadili na kupitia hoja za Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kilichofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.

Amesema hakuna sababu ya halmashauri kuendelea kuwa na hoja zinazoweza kuepukika kutokana na uzembe au ukosefu wa usimamizi madhubuti, Amesisitiza kuwa madiwani wanapaswa kutumia mamlaka yao ipasavyo kuhoji, kufuatilia utekelezaji wa maelekezo na kuhakikisha hoja zote za ukaguzi zinafungwa kwa wakati, sambamba na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali Mussa, amehimiza halmashauri kuendelea kutekeleza programu ya Jisomeshe na Mkarafuu, akieleza kuwa mpango huo utasaidia kupunguza utegemezi wa ajira kwa vijana kwa kuwawezesha kujiajiri kupitia kilimo cha karafuu. Pia amesisitiza umuhimu wa kuendelea kugawa miche ya zao hilo ili kuongeza uzalishaji, kuinua kipato cha wananchi na kukuza uchumi wa Mkoa wa Morogoro.

Naye mwakilishi wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Stephen Kassaro, amesema moja ya hoja zinazochelewa kufungwa ni ile ya urejeshaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu,Amesema kiwango cha marejesho bado hakiridhishi, hivyo amewataka madiwani kutembelea vikundi vinavyonufaika na mikopo hiyo ili kubaini changamoto zinazokwamisha marejesho na kuwezesha fedha hizo kuendelea kuwanufaisha walengwa wengine.

Akihitimisha kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Kibena Kingo, amesema madiwani wamepokea maelekezo yote yaliyotolewa na kuahidi kuyatekeleza kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato, kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo na kushirikiana kwa karibu na watumishi wa halmashauri kwa lengo la kuboresha huduma na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!