Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amezionya taasisi za umma na binafsi pamoja na wasaidizi wake wanaoshindwa kuwapa wajasiriamali wadogo fursa ya kuwekeza na kufanya biashara katika maeneo yao na kwamba hatavumilia vitendo vyote vyote vya kuwakwamisha wawekezaji wanaotaka kuwekeza mkoani humo.
Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Morogoro, Malima amesema kuwa kundi la wajasiriamali wadogo ni muhimu sana katika uchumi wa mkoa na taifa, hivyo lazima wawe wanapewa kipaumbele katika upatikanaji wa maeneo ya biashara, mikataba, na huduma mbalimbali ili waweze kukua kiuchumi.
Aidha, ameziagiza halmashauri zote za mkoa wa Morogoro kuhakikisha zinatoa kazi na tenda kwa baadhi ya vikundi vya wajasiriamali vinavyokopa mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, ili kuwarahisishia kurejesha mikopo hiyo kwa wakati na kukuza mitaji yao.
Malima ameongeza kuwa eneo la biashara linahitaji mabadiliko na mitazamo chanya ili kila mdau aone umuhimu wa kuwezesha makundi madogo ya kiuchumi kupata fursa za kiuchumi na si fursa hizo kwenda kwa wachache walio na nguvu za mitaji mikubwa.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, sekta binafsi, wakuu wa wilaya, wajasiriamali pamoja na wawakilishi wa vikundi vya kijamii, kwa pamoja walijadili namna ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji mkoani Morogoro.