Latest Posts

RC MTAMBI: NINATAMANI SGR IFIKE MKOA WA MARA DIRA 2050

Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi ameongoza majadiliano yaliyohusisha wananchi na viongozi kuelekea maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025-2050.

Akizungumza kwenye kikao maalumu cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika Agosti 19, 2024 kwenye ukumbi wa uwekezaji amesema tayari majadiliano hayo yamefanyika ngazi ya wilaya na sasa ni mkoa kabla ya kupelekwa maoni ngazi ya taifa kwenye Tume ya Mipango.

Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo ni suala la msingi katika masuala mbalimbali hivyo mkoa unayo nafasi ya wananchi na viongozi kujadiliana.

Mtambi amesema lengo la kikao hicho ni kutoa fursa kwa wananchi na viongozi wa mkoa wa Mara kutoa maoni yao kuhusu Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 ambayo ipo katika hatua za maandalizi.

“Dira inaonesha matamanio na vipaumbele vya wananchi, serikali na taasisi binafsi zinapotamani kufikia kwa muda flani na mipango mbalimbali inawekwa ili kufikia lengo hilo”, amesema Mtambi.

Kanali Mtambi amesema Tume ya Mipango imewasilisha katika Mkoa wa Mara maelekezo ya namna ya kukusanya maoni, mapendekezo na ushauri ili wananchi, viongozi na taasisi zitoe maoni kwa ajili ya dira hiyo.

Amesema kwa kawaida nchi inakuwa na mipango ya muda mrefu, muda wa kati na muda mfupi na utekelezaji wake unaweza kulitoa taifa kutoka katika eneo moja kwenda eneo lingine.

RC Mtambi amesema anatamani katika mipango ya miaka ijayo reli ya kisasa ya SGR iwe imefika mkoa wa Mara kutokea Arusha au Mwanza ili kurahisisha usafiri kwa watu na mizigo kutoka katika mkoa wa Mara na kuinua uchumi.

Akizungumza katika kikao hicho Naibu Waziri wa Sheria na Katiba Jumanne Sagini amesema mkoa wa Mara umepiga hatua kubwa katika miundombinu ya barabara ambapo hapo awali wananchi walikuwa wanatumia zaidi usafiri kupitia nchi za Kenya na Uganda wakati wa kwenda Dar es Salaam na mikoa mingine.

Sagini ameshauri mkoa utilie mkazo kuhusu urejeshaji wa bandari ya Musoma ili iweze kufanya kazi kuunganisha na treni ya SGR ambayo inatarajiwa kufika mkoa wa Mwanza na hivyo itasaidia katika usafirishaji wa mizigo na kurahisisha upatikanaji wa bidhaa.

Naye Mbunge wa jimbo la Musoma Vijijini Profesa Sospeter Muhongo amesema wakati taifa linatoa maoni ni vizuri wataalamu wa mipango wakajiuliza wakati huo Dira inapotekelezwa Tanzania itakuwa na watu wangapi, dunia pia itakuwa na watu wangapi ili kupanga mipango yenye uhalisia.

Prof. Muhongo amesema katika mwaka wa 2050 Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni 120 hadi 141 ambao ni zaidi ya mara mbili ya watu waliopo sasa na mipango yote inatakiwa kuwekwa kwenye mahesabu watu hao ili Tanzania isipange mipango kwa ajili ya watu wachache wakati inakadiriwa kutakuwa na watu wengi.

Ametolea mfano wa umeme na kusema kuwa kwa sasa umeme unatosheleza kwa kuwa bado idadi ya watu, viwanda na ofisi ni ndogo ukilinganisha na wakati huo, na kutahadharisha kuwa ili kuwa na umeme wa uhakika wa wakati huo ni lazima kuangalia mahitaji halisi ya umeme kwa wakati huo na sio hali ya sasa hivi tu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!