Serikali kupitia Wizara ya Afya imesaini makubaliano ya ushirikiano (MoU) na kampuni ya kimataifa ya Abbott, maarufu kwa huduma na bidhaa za afya, yenye lengo la kuchunguza uwezekano wa kutengeneza vipimo vya haraka vya magonjwa mbalimbali hapa nchini.
Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Dodoma ambapo Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, amesema kuwa serikali imejipanga kuongeza uzalishaji wa bidhaa za afya ndani ya nchi ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.
“Tunaelekea katika mwelekeo sahihi. Moja ya vipaumbele vyetu ni kuongeza uzalishaji wa bidhaa za afya nchini. Tunashukuru sana kwa uwekezaji huu,” amesema Waziri Mhagama.
Amesema kuwa kuanzishwa kwa kiwanda cha kutengeneza vipimo vya magonjwa kama UKIMWI, kaswende na homa ya ini kutaiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha huduma bora za afya katika kanda, sambamba na kupunguza gharama na kuongeza upatikanaji wa vipimo hivyo kwa urahisi.
Aidha, Waziri Mhagama alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kuboresha huduma za afya kwa kutumia teknolojia ya kisasa na mifumo ya kidijitali ili kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Steven Henn kutoka kampuni ya Abbott amesema kuwa ushirikiano huo unaonesha dhamira ya kampuni yao katika kuboresha huduma za afya kwa Watanzania na nchi za jirani.
Naye Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi, amesema kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo utasaidia kupunguza gharama kubwa ambazo serikali ilikuwa ikitumia kuagiza vipimo kutoka nje ya nchi.
“Fedha hizo zilikuwa zikitumika kununua vipimo vya UKIMWI, homa ya ini na kaswende kwa lengo la kusaidia kudhibiti maambukizi zaidi miongoni mwa wananchi,” amesema Msasi.