Tanzania iko mbioni kuandika historia mpya katika ramani ya filamu kupitia tamasha jipya lenye hadhi ya kimataifa – Tamasha la Filamu la Kilimanjaro, (Kilimanjaro Film Festival – KFF2025). Likitarajiwa kufanyika kuanzia 02 hadi 06 Julai 2025, tamasha hili litafanyika chini ya kivuli cha Mlima Kilimanjaro, mlima maarufu na mrefu zaidi barani Afrika. Ni jukwaa linalowaunganisha wasanii wa filamu, vijana wabunifu, wadau wa utamaduni na wageni wa kimataifa kutoka pande zote za dunia wataungana kwa ajili ya kusherehekea hadithi, tamaduni na uzuri wa bara letu kupitia filamu.
Kwa jina lenye uzito wa kipekee, tamasha hili linaibuka kama harakati ya kuandika upya simulizi za Afrika kwa sauti zetu wenyewe. Ni fursa adhimu ya kuonesha uzuri, ustaarabu, changamoto na mafanikio ya bara letu kwa kutumia filamu kama daraja la mabadiliko na maendeleo. Linakuja na nguvu mpya, shauku kuu na dhamira ya kulifanya filamu kuwa chombo chenye athari chanya kijamii, kiuchumi na kimazingira.

KFF2025 si tukio la burudani tu. Ni uwanja wa mazungumzo ya maana, mahali ambapo masimulizi ya wanawake waliopuuzwa, changamoto za mabadiliko ya tabianchi, fursa kwa vijana na uzingatiaji wa tamaduni zetu huwekwa mezani kwa njia ya kisanaa. Kwa kauli mbiu ya “Ulimwengu wa Afrika”, tamasha linalenga kutumia filamu kama jukwaa la maelewano, mshikamano na ujenzi wa jamii yenye fahari na sauti ya pamoja.
Tamasha hili linakusudia kuunganisha utalii na filamu. Kupitia tamasha hili, washiriki kutoka sehemu mbalimbali wataweza kutangaza uzuri wa Tanzania huku wakirekodi hadithi zao za ushindi, uthubutu na maono. Kuanzia 28 Juni hadi 06 Julai, kutakuwa na Sanaa Soko, ambalo ni jukwaa la mauzo ya kazi mbalimbali za sanaa ikiwa ni pamoja na picha, mavazi ya asili, chakula, na bidhaa za kiubunifu kutoka kwa makundi mbalimbali ya wabunifu wa Tanzania. Sambamba na hilo, Maonyesho ya Uhifadhi wa Jamii yataonyesha miradi ya uhifadhi inayotekelezwa na jamii mbalimbali. Katika kuunganisha mzunguko wa utalii, Zanzibar itashiriki kipekee kwa kuonesha filamu mbalimbali zinazosadifu mandhari ya kiutamaduni kutoka visiwani.
Kwa kuzingatia umuhimu wa ushirikishwaji, tamasha litatoa nafasi kwa jamii kushuhudia filamu zenye maudhui ya jamii zao, huku Kilimanjaro Film Lab ikiwapa vijana mafunzo ya vitendo ya uandaaji wa shughuli za ubunifu, utengenezaji wa filamu, uhariri, uandishi na matumizi ya teknolojia mpya.
Tarehe 02 Julai, kutafanyika Sherehe ya Ufunguzi wa KFF2025 kuanzia saa 12 jioni, ikiambatana na maonyesho ya filamu kwa umma hadi usiku wa manane. Hii ni fursa ya wadau wa filamu, wageni wa kimataifa na wananchi wa kawaida kushuhudia uzinduzi rasmi wa tamasha hili jipya kwa shangwe na mbwembwe.
Tamasha pia limeandaa warsha na midahalo yenye lengo la kukuza uelewa na kushirikisha ujuzi wa filamu kwa kuangazia mjadala wa filamu na mandhari ya Tanzania, uhusika wa wanawake katika kujenga simulizi imara za Afrika. Watoto pia hawajaachwa nyuma. Kutakuwa na warsha ya usimuliaji hadithi kwa watoto ili kuweza kujenga msingi imara kwenye jamii ambapo watoto wanathaminiwa kama sehemu ya utunzaji wa kumbukumbu za jamii.
Kilele cha tamasha kitafanyika tarehe 6 Julai 2025, siku ambayo itajumuisha matukio matatu makubwa. Soko la Maudhui (Content Market) ambapo litafungua siku kwa kutoa fursa kwa watayarishaji wa filamu kuonyesha kazi zao, kupata wawekezaji, wabia na fursa za masoko ndani na nje ya nchi.
Jioni yake, kuanzia saa 12, kutafanyika Sherehe ya Tuzo za Kilimanjaro Tanzanite ambayo inalenga kutambua wadau, washirika, vipaji na kazi bora zilizojitokeza wakati wa tamasha. Tuzo hizi ni sehemu ya kutambua uwekezaji na mafanikio katika sekta ya filamu Tanzania kwa ujumla wake.Tamasha litahitimishwa kwa burudani mbalimbali kwa wabunifu, wageni, na wadau wote walioshiriki kwenye tamasha hilo la kipekee.
Kilimanjaro Film Festival, ni zaidi ya tamasha la filamu. Ni jukwaa la kuonesha utu, historia, mapambano na ndoto za bara letu. Ni nafasi ya kusimulia simulizi zetu sisi wenyewe – kwa ufahari, uzalendo na ubunifu wa hali ya juu. Tamasha hili litakuwa linafanyika kila mwaka kuanzia tarehe 2-6 Julai ili kuendeleza malengo yake ya kuweka tasnia ya filamu sambamba na utalii. Wadau mbalimbali wanakaribishwa kushiriki na kuwa sehemu ya historia hii ya filamu Tanzania
Karibu Kilimanjaro. Karibu KFF2025. Karibu kusimulia ulimwengu wa Afrika!
Kwa taarifa zaidi tembelea tovuti hii hapa