Latest Posts

TAMESOT YASISITIZA KILA MGANGA WA TIBA ASILI AWE NA LESENI “ITAPUNGUZA UHALIFU”

Na Theophilida Felician.

Chama cha Waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala Tanzania (TAMESOT) kimetoa wito kwa vyombo vya dola kuwachukulia hatua watu wanaojihusisha na huduma za tiba asili bila vibali halali, kikisema kwamba matukio ya kihalifu yanayohusishwa na waganga hao yanaichafua sekta hiyo na kupunguza imani ya jamii.

Katibu wa TAMESOT Taifa, Lukas Joseph Mlipu, alisema hayo akizungumza kwa njia ya simu akiwa mkoani Dodoma, ambapo alisisitiza kuwa watu hao ni matapeli wanaojificha katika sekta ya tiba asili kufanya uhalifu.

 

“Mganga halali ni yule mwenye leseni. Asiyekuwa nayo si mganga bali ni tapeli. Wamevamia sekta hii, wamechonganisha waganga halali na wananchi, na matokeo yake ni kupungua kwa imani na kuongezeka kwa maumivu ya kijamii,” alisema Mlipu.

Aidha, Mlipu aliiomba wizara ya afya kupitia Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kusimamia kikamilifu utoaji wa leseni na kusajili tu wale wanaokidhi vigezo vya kitaaluma na maadili ili kuondoa mianya ya kihalifu.

Katika mahojiano hayo, Katibu huyo alilaani vikali tukio la kukamatwa kwa watu wawili mkoani Kagera waliokutwa na viungo vinavyodhaniwa kuwa vya binadamu, akisema tukio hilo linaweza kuhusishwa na matumizi mabaya ya jina la tiba asili.

“Hatuwezi kukaa kimya. Tunatoa pole kwa familia zilizoathirika, na tunaliomba Jeshi la Polisi liendelee na operesheni ya kuwasaka wahusika wote wa aina hii, hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi ambapo mambo mengi huibuka,” alisema.

Pamoja na hayo, Mlipu ametoa wito kwa Serikali kuipa sekta hiyo sauti kwenye vyombo vya maamuzi hasa kwa kuwajumuisha waganga halali kwenye viti maalum vya Bunge, akisema kuwa kufanya hivyo kutasaidia kutunga sera bora za kuimarisha tiba asili nchini.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!