Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonesha kuridhishwa na mafanikio katika sekta ya kahawa kufuatia uwekezaji uliofanywa na serikali katika kilimo.
Akizungumza Jumanne, Septemba 24, 2024, wakati wa ziara yake kwenye shamba la kahawa la Aviv Tanzania Limited mkoani Ruvuma, Rais Samia ameeleza kuwa uzalishaji wa kahawa umeongezeka kutoka wastani wa tani 65,000 hadi zaidi ya tani 80,000, ongezeko ambalo lina manufaa makubwa kwa uchumi wa taifa.
“Hili ongezeko la uzalishaji wa kahawa linatuongezea pato la kigeni. Kwa mwaka huu tunatarajia mauzo ya kahawa nchini kuingiza dola milioni 250,” amesema Rais Samia. Amebainisha kuwa kiasi hicho ni sawa na msaada au mkopo ambao serikali imekuwa ikiuomba kutoka nje, mara nyingi kwa masharti.
Rais Samia alieleza kuwa fedha zinazopatikana kupitia mauzo ya kahawa zina umuhimu mkubwa kwani zinasaidia kupunguza utegemezi wa misaada ya kigeni.
“Kwa kawaida, mimi huwa ninapiga magoti na kuomba misaada ya kiasi hiki. Sasa kama tunaweza kuzalisha dola milioni 250 kutoka kwenye zao moja tu la kahawa, tunapaswa kuimarisha jitihada zaidi ili tuzalishe zaidi ya hapa,” amesisitiza.
Rais Samia pia ameeleza matarajio ya serikali kuongeza uzalishaji wa kahawa mara mbili zaidi katika kipindi cha miaka mitano ijayo, huku akihimiza ushirikiano na sekta binafsi na wawekezaji ili kufanikisha malengo hayo.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kujitegemea kiuchumi kupitia kilimo kwamba ikiwa Tanzania itazalisha yenyewe, fedha zitakwenda moja kwa moja nchini bila masharti yoyote kutoka nje.