Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Telack amezitaka taasisi zote zinazohusika katika usafirishaji wa korosho kupitia bandari ya Mtwara kuhakikisha zinatekeleza majukumu yao ipasavyo ili korosho zisafirishwe kwa wakati bila kuwepo vikwazo vyovyote.
Akizungumza Septemba 19, 2024 kwenye Mkutano wa Wadau wa Bandari ya Mtwara (maandalizi ya msimu wa korosho 2024, 2025) amesema ili kuepuka vikwazo lazima taasisi zote zinazosafirisha korosho zitekeleze majukumu yake kwa wakati.
Ameongeza kuwa mwaka jana msimu wa korosho 2023, 2024 tani laki 250,000 zilisafirishwa kupitia bandari ya Mtwara hivyo amesisitiza kutokuwepo kisingizo chochote cha kurudisha nyuma usafirishaji wa korosho kupitia bandari hiyo.
Hata hivyo Zainab Telack ameagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) mkoa wa Mtwara kuelekea kwenye msimu wa korosho 2024, 2025 kujitathimini na kujipanga ili msimu utakapoanza kusiwepo na maneno bali viwepo vitendo na waweze kutimiza malengo waliojiwekea ya kusafirisha tani laki 500,000.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa TPA Dkt. George Fasha amesema kwa msimu huu hakutakuwa na changamoto ya kuhudumia korosho kwa upande wa bandari kwani hadi sasa bandari ya Mtwara ina gati mbili kubwa, ina eneo la kutosha kuhifadhia makasha matupu na yenye shehena, ina mzani wa kupimia shehena, ina mdaki (scana) wa kukoboa shehena, na ina mitambo mikubwa na kisasa ya kutosha kuhudumia shehena ya makasha.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Bahati Geuzye amesema wao kama sekretarieti ya mkoa wanaendelea kusimamia shughuli hizo za kilimo pamoja na kuwahimiza wananchi kulima mazao mengine licha ya kuwa zao la korosho kwa mkoa huo ndiyo zao ambalo wananchi wanalitegemea sana.