Katika mwendelezo wa kampeni ya utoaji elimu kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa hiyari, Afisa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Iringa, Shaga Gagunda, alifika kijiji Cha Migoli, kata ya Migoli ya wilaya ya Iringa kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi wa eneo hilo.
Katika mkutano huo, Afisa Gagunda aliwafafanulia wananchi umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari, akisisitiza kuwa kodi ndio nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa. Alieleza jinsi kodi inavyosaidia katika utoaji wa huduma za msingi kama vile afya, elimu, na miundombinu, huku akihimiza wafanyabiashara kuhakikisha wanazingatia sheria za kodi kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Baada ya kupokea elimu hiyo, wananchi walipata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali kuhusu kodi, huku baadhi yao wakionyesha shauku ya kufahamu zaidi kuhusu taratibu za ulipaji kodi na namna ya kusajili biashara zao rasmi. Kwa upande wake, Afisa Gagunda alitoa majibu ya kina na kuendelea kutoa huduma kwa wafanyabiashara waliokuwa na mahitaji maalum. Miongoni mwa waliopata huduma hiyo ni wafanyabiashara wapya ambao walipatiwa namba za utambulisho wa mlipakodi (TIN) kwa ajili ya biashara zao.
Wakizungumza mara baada ya kupokea elimu hiyo, baadhi ya wafanyabiashara walitoa maoni yao, wakieleza kuwa wamepata uelewa mpana kuhusu umuhimu wa kulipa kodi na kwamba elimu hiyo imewasaidia kufahamu taratibu zinazopaswa kufuatwa ili kuepuka migogoro na mamlaka za kodi.
“Kwa kweli elimu hii imetufungua macho, tumeelewa umuhimu wa kulipa kodi kwa hiyari na sasa tupo tayari kushirikiana na TRA kwa ajili ya maendeleo ya biashara zetu,” amesema mmoja wa wafanyabiashara hao.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kijiji cha Migoli, Majeshi Richard, alieleza kuwa elimu hii itasaidia kupunguza malalamiko na misuguano kati ya wananchi na serikali kuhusu masuala ya kodi. Alisisitiza kuwa uelewa mzuri wa sheria za kodi utarahisisha mahusiano kati ya wafanyabiashara na mamlaka husika, hivyo kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Elimu ya ulipaji kodi kwa hiari inaendelea kutolewa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Iringa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za TRA kuhakikisha kuwa kila mfanyabiashara anakuwa na uelewa sahihi wa wajibu wake wa kulipa kodi na faida zake kwa taifa.