Rais wa Marekani Donald Trump ameziambia nchi zinazouza mafuta zinazounda Shirika la Nchi Zinazozalisha Petroli (OPEC), hasa Saudi Arabia, kupunguza bei ya mafuta, akiongeza tishio la kuanzisha kodi za ziada iwapo hakutakuwa na hatua za haraka.
Trump amesema kuwa bei za juu za mafuta zinatoa msaada wa kifedha kwa vita vya Urusi na Ukraine, hali ambayo alisema inahitaji kudhibitiwa mara moja.
Kauli yake ilishusha bei ya mafuta ghafi kwa 1% mara baada ya kutolewa. David Oxley, mtaalamu wa uchumi wa bidhaa, alisema kuwa maoni ya Trump yanaendana na dhamira yake ya kupunguza bei za mafuta kama mkakati wa kushinikiza Urusi kumaliza vita vya Ukraine. Hata hivyo, ameonya kuwa bei ya chini ya mafuta inaweza kuathiri wazalishaji wa mafuta wa Marekani, hasa katika maeneo yenye gharama kubwa kama Alaska.
Trump pia amesema kuwa atamuomba Mfalme Mohammed bin Salman wa Saudi Arabia kuongeza uwekezaji wa nchi hiyo nchini Marekani hadi kufikia dola trilioni 1, hatua inayolenga kuimarisha uchumi wa Marekani. Amesisitiza kuwa serikali na kampuni za kimataifa zinapaswa kutengeneza bidhaa zao ndani ya Marekani ili kuepuka kodi kubwa, akionesha azma yake ya kulinda viwanda vya ndani.
Pia ameitaka serikali ya Marekani kupunguza viwango vya riba ili kukabiliana na matatizo ya kiuchumi ambayo alisema yamesababishwa na sera za utawala wa Rais Joe Biden.
Trump amezungumza kuhusu matumizi ya makaa ya mawe kama chanzo cha nishati, akisema kuwa Marekani inahitaji kuongeza uzalishaji wa nishati ili kuhimiza maendeleo ya teknolojia kama akili mnemba (artificial intelligence).
Kauli hizo zimetolewa katika Mkutano wa Uchumi wa Dunia, ambapo Trump amezungumza kwa mara ya kwanza na hadhira ya kimataifa tangu kuapishwa kwake wiki hii.