Latest Posts

TUSHIYA FOUNDATION YAJIPANGA KUIMARISHA UCHUMI WA VIJANA TANZANIA

Katika kujikwamua kiuchumi, vijana wa Kitanzania wamekuwa wakikumbwa na changamoto mbalimbali hasa katika kupata ajira na kuweza kudumu katika ajira hizo.

Moja ya sababu zinazoelezwa kuchochea changamoto hizo ni ukosefu wa ujuzi unaohitajika katika kazi, bidii hafifu kazini na ukosefu wa uaminifu. Hata hivyo, kila tatizo lina kiini chake na kitakapopatikana kiini hicho basi mwanzo wa utatuzi unapatikana.

Vijana John Waryuba, Bonami Kyunda na Haggai James wameamua kuanzisha taasisi ambayo itahusika kuwakwamua vijana kuondokana na changamoto za kiuchumi huku suala la fikra na mtazamo wa namna vijana wanavyoyaona mambo vikipewa kipaumbele, taasisi hiyo inajulikana kama Tushiya Foundation.

Waryuba ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa taasisi amesema wanahitaji kuona vijana wanapata ajira, na wale wenye ajira waweze kudumu katika ajira na uchumi.

Amesema malengo makubwa ya taasisi hiyo ni kuona vijana wanawajibika, wawe na kitu cha kufanya kitakachowaongezea kipato kwa ajili ya matumizi ya kila siku, na kuhifadhi akiba kwa ajili ya dharura katika siku za usoni.

Aidha ameeleza kuwa watakuwa na programu nyingi zitakazosaidia vijana kujitegemea na kuitumikia nchi ya Tanzania kupitia kodi zitakazotozwa kutokana na ajira watakazopata.

“Kama Tushiya Foundation, lengo letu ni kuimarisha maendeleo ya kiuchumi ya vijana kupitia mafunzo, uhamasishaji na miradi ya kiuchumi inayolenga kuendeleza uwezo wao wa kujitegemea na kuchangia katika uchumi wa jamii na taifa”, ameeleza Waryuba.

Aidha wamesema kuwa vijana watakuwa wakipewa fursa za ajira na ujasiriamali kupitia programu zake mbalimbali ambazo zitakuwa katika mifumo ya warsha, midahalo, vipindi vya runinga na kadhalika.

Kwa upande wake Kyunda ambaye ni katibu wa taasisi hiyo amesema kuwa wao kama vijana wamelenga kuakisi vijana kwa kiasi kikubwa, hivyo wamewaomba wadau mbalimbali ikiwamo vijana wenyewe, wazazi na serikali kuwaunga mkono katika safari hiyo ya kumkwamua kijana wa Kitanzania.

Naye Mratibu wa Tushiya Foundation, Haggai amesema kupitia programu mbalimbali zitazotolewa na taasisi hiyo vijana watapewa nafasi ya kujifunza namna ya kuratibu na kusimamia mitaji wanayoipata, nidhamu ya fedha na mengine mengi ambayo yatasaidia vijana ambao ni kundi kubwa la watu nchini Tanzania kujikwamua kiuchumi, hivyo kuakisi kile kinachoitwa uchumi jumuishi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!