Shirika lisilo la kiserikali la Grumeti Fund limeadhimisha Siku ya Twiga kwa kutoa wito kwa Serikali na wadau wa uhifadhi kuongeza juhudi za kumlinda mnyama Twiga, ambaye ni nembo ya Taifa la Tanzania, lakini kwa sasa yuko katika hatari ya kutoweka kutokana na vitisho kadhaa vinavyoongezeka siku hadi siku.
Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika Wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara, viongozi wa Grumeti Fund wamesema kuwa Twiga, licha ya upole wake na umuhimu wake kwa Taifa, amekuwa miongoni mwa wanyamapori wanaoendelea kushambuliwa kwa uwindaji haramu, ukosefu wa malisho, shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi, ukame, pamoja na imani potofu zinazodai viungo vyake vinaweza kutumika katika tiba.

Kwa mujibu wa IUCN (Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira), duniani kwa sasa wapo takriban Twiga 117,000, huku Tanzania ikitajwa kuwa na zaidi ya Twiga 23,000. Aidha, utafiti wa mwaka 2009 wa Tanzania Wildlife Research Institute (TAWIRI) unaonesha kuwa Twiga wa Masai pekee wanakadiriwa kufikia 28,850 nchini.
Katika juhudi za kulinda mnyama huyo, Grumeti Fund imeanzisha programu maalum ya elimu kwa watoto mashuleni, ili kuwajengea uelewa wa umuhimu wa uhifadhi wa Twiga na viumbe hai wengine.

Twiga ni mnyama mpole asiye na tabia ya kushambulia, hali inayomfanya kuwa miongoni mwa wanyama rahisi kudhurika. Aidha, ni almasi ya utalii, kivutio kikuu kwa wageni wanaotembelea hifadhi mbalimbali nchini. Hata hivyo, vitisho vinavyoendelea kuongezeka vinaweza kupelekea mnyama huyu kupotea kabisa katika miaka michache ijayo.