Latest Posts

UCHAGUZI WA S/MITAA NA WASIWASI WA UPINZANI KUJITOKEZA ‘MADUDU’ YA MWAKA 2019

Mchaka mchaka wa uchaguzi wa serikali za mitaa unaendelea hapa nchini huku kwa sasa kinachosubiriwa zaidi ikiwa ni kuanza kwa mbiringe mbiringe za kampeni ambapo itashuhudiwa wagombea wa nafasi mbalimbali wakinadi sera zao majukwaani

Hata hivyo, kabla ya kuelekea huko kwa sasa kumekuwa mjadala mpana sana unaoendelea hapa nchini ambao kwa namna moja au nyingine mjadala huo unaonesha taswira hasi kuhusiana na muenendo wa uchaguzi wenyewe, na pengine huenda kama mambo yakawa hivyo kama inavyosemwa basi sio dhambi kusema uchaguzi huu utakuwa umegubikwa na dosari kubwa

Hivi karibuni nimefuatilia kwa karibu mkutano wa wanahabari uliokuwa umeitishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tanzania Bara Benson Kigaila na Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini Godbless Lema, mkutano uliofanyika jijini Arusha ambapo msingi wa mkutano ule ulikuwa ni kuueleza umma kupitia wanahabari muenendo wa uchaguzi huo

Katika makala hii, nitajikita kugusia angalau kwa uchache yale yaliyozungumzwa na Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini Godbless Lema katika mkutano huo, Lema alijikita kueleza kasoro na dosari kadha wa kadha zilizojitokeza kwenye Kanda ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Arusha, Tanga, Kilimanjaro na Manyara

Katika maelezo yake amedai kuwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi mbalimbali wakiongozwa na Wakurugenzi wa Halmashauri wamekuwa wakiwaengua wagombea wa vyama vya upinzani kinyume na taratibu na kwamba hali hiyo kwa kiasi kikubwa inatishia ustawi wa uchaguzi wenyewe

Amesema hadi kufikia sasa zaidi ya asilimia 70 ya wagombea wao wameingia kwenye kadhia hiyo iwe kwa kuwekewa mapingamizi ya ‘mchongo’, kutishiwa au kuenguliwa kabisa

Akitolea mfano wa jambo hilo Lema ameitaja wilaya ya Same kuwa ni miongoni mwa maeneo ambayo wagombea wa CHADEMA karibu wote walienguliwa huku wengi wao wakienguliwa kwa madai ya kwamba jina la chama chao wameandika CHADEMA badala ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo, hatua iliyopelekea yeye binafsi baada ya kupata taarifa hiyo kuchukua hatua za ziada za kuwasiliana na Mkurugenzi wa Same, Mkuu wa wilaya ya Same na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro ambapo aliwatahadharisha kuwa katu hawatakubali ‘uonevu’ huo

Amesema kanuni za uchaguzi huo zimeeleza wazi kuwa mgombea anaweza kuandika jina la chama chake kwa kifupi au kirefu na hiyo yote inakubalika, ndio maana yeye binafsi amedai kuwa amezishuhudia fomu nyingi za wagombea wa tawala zikiwa zimeandikwa CCM badala ya Chama cha Mapinduzi lakini hazijawekewa pingamizi lolote kwa kuwa wanaamini ziko sawa

Inaelezwa baada ya Lema kuwasiliana na viongozi hao wa wilaya ya Same na mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla wake, baadaye ikashuhudiwa Mkurugenzi mtendaji wa Same akitoa tangazo la kueleza kuwa wagombea wote walienguliwa ndani ya Halmashauri hiyo wamerejeshwa kugombea na kwamba hakuna pingamizi lolote kwa mgombea yeyote, hata hivyo kadhia kama hiyo kwa mujibu wa Lema amedai kuwa imetokea kwenye maeneo mengi ya kanda hiyo na kwenye maeneo mbalimbali ya nchi

Ametolea mfano mwingine kuwa ni ule uliotokea kwenye kata moja wilayani Handeni, mkoani Tanga ambapo Mkurugenzi mtendaji aliwakabidhi karatasi wagombea na kuwaeleza kuwa wanapaswa kuandika kile anachokiongea yeye akidai kuwa lengo la kufanya hivyo ni kupima uwezo wa kujuwa kusoma na kuandika kwa wagombea jambo ambalo halikubaliki na kinyume cha kanuni za uchaguzi huo, sambamba na hilo Lema amedai kuwa Mkurugenzi kwa nafasi yake hausiki kwenye uwekaji wa mapingamizi kwa kuwa yeye ni mamlaka ya rufaa katika uchaguzi huo

Godbless Lema ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA ameenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa ‘madudu’ yanayotokea katika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 kwa kiasi kikubwa yanazidi ‘madudu’ yaliyoshuhudiwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 ambapo vyama kadhaa vya upinzani ikiwemo CHADEMA na ACT Wazalendo vilisusia uchaguzi huo kutokana na idadi kubwa ya wanachama wake kuenguliwa

Kauli hiyo ya Lema inasindikizwa kwa kiasi kikubwa na chapisho liliwekwa na Kiongozi wa zamani wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe kwenye kurasa zake binafsi za mitandao ya kijamii ambaye kwa kiasia kikubwa naye amegusia jambo hilo kuwa mlolongo wa wagombea wa upinzani kuenguliwa unatishia ustawi wa uchaguzi huo

Zitto anasema kwa takribani siku tatu (3) sasa amekuwa akipokea taarifa lukuki na takwimu kuhusu kuongezeka kwa namba za wagombea wa vyama vya upinzani wanaoenguliwa kutoka kwenye vitongoji, vijiji na mitaa kwenye kila kona ya nchi

Zitto ameenda mbali zaidi kwa kusema kuwa awali aliamini kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka huu (2024) utakuwa na mazingira rafiki na kwamba kwa kiasi kikubwa utafukia mashimo yote yaliyojiyokeza kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019, jambo ambalo limekuwa tofauti

Katika kuchochea ajenda ya mageuzi na kile kilichoonekana kama kutoa tahadhari kwa viongozi na wafuasi wa vyama vya upinzani nchini Zitto ametaka kwa umoja wao kuamka na kuchukua hatua kwa kuwa katu wasitarajie kuwa mazingira ya uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 yatakuwa kama yale ya mwaka 2014 ambapo inatajwa kuwa vyama vya upinzani vilifanya vizuri kwa kuwa angalau kwa kiasi fulani viliwekewa mazingira rafiki

Huu ni mfululizo wa malalamiko kutoka kwenye vyama vya upinzani hususani vyama vikuu vya upinzani katika nchi yetu ambavyo ni CHADEMA, ACT Wazalendo na CUF ambavyo kwa nyakati tofauti vimejitokeza kueleza ‘madudu’ yaliyoko kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa 2024

Malalamiko ya uchaguzi huo yameanza kujitokeza tangu awali pale ilipobainika kuwa OR-TAMISEMI ndio inayoratibu na kusimamia uchaguzi huo, naheshimu maamuzi ya kisheria yaliyoamuliwa Mahakamani hivi karibuni kuhusu suala hilo lakini wasiwasi uliokuwa unalalamikiwa unaweza kupigiwa tiki na wadau pindi wanapoona mambo hayaendi sawa, huku ikifahamika kuwa miongoni mwa malalamiko yao ni pamoja na kwamba Waziri wa ofisi hiyo ambaye ndio msimamizi mkuu wa uchaguzi huo ni mwanasiasa wa chama tawala (CCM), Waziri ambaye ni mteule wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kama hiyo haitoshi Rais aliyemteua Waziri na kumuapisha ni Mwenyekiti wa chama tawala Taifa, hivyo mashaka ya wengi yalikuwa ni uwepo wa mgongano wa maslahi

Wakati wa zoezi la kuandikisha daftari la mkazi malalamiko yaliongezeka zaidi hapa kwa kiasi kikubwa wengi wakilalamikia ‘madudu’ lukuki ikiwemo kuandikishwa kwa wanafunzi na watoto ambao hawajakidhi umri wa kuandikishwa kwenye daftari hilo, madai ya kuandikishwa kwa watu waliokufa au kupotea, uwepo wa idadi kubwa ya takwimu ya watu walioandikishwa kuliko uhalisia hapa ikidaiwa kuwa huenda takwimu husika ‘imepikwa’ nk, na sasa malalamiko hayo yamefikia hatua ya mapingamizi

Lakini kama hiyo haitoshi, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Mnyika, kupitia ukurasa wake binafsi wa mtandao wa X (twitter) amechapisha ujumbe unaosomeka hivi; “Rais @SuluhuSamia na Waziri Mchengerwa @ortamisemitz naamini mna taarifa juu ya hujuma zinazoendelea katika halmashauri nyingi baada ya zoezi la kurudisha fomu kukamilika tarehe 1 Novemba 2024”

“Wakurugenzi ambao ni wasimamizi wa uchaguzi wako mstari wa mbele kwa kushirikiana na Wakuu wa wilaya na maofisa usalama wa wilaya kutoa maelekezo kwa watendaji wa kata, mitaa na vijiji ambao ndio wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi juu ya namna ya kuengua kwa wingi wagombea wa @ChademaTz tarehe 8 Novemba wakati wa uteuzi kwa sababu za uongo na kuanzia tarehe 9 Novemba 2024 kupitia mapingamizi haramu” -Mnyika

“Uchakachuaji mlioufanya kwenye uandikishaji wa wapiga kura na ukwamishaji wa baadhi ya wagombea mmeona bado hautoshi mpaka mmeamua kurudia kwa ukamilifu wake udhalimu kama ule wa 2019?, msitulaumu kwa yatakayotokea” -Mnyika

Jambo TV inazo taarifa fiche za kuaminika kutoka kwenye vyanzo vya ndani ya baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani kuwa kwa sasa vikao vya majadiliano vinaendelea ili waweze kuona namna watakavyoukabili uchaguzi huo katika mazingira ambayo wanadai kuwa si rafiki kwao, huku ikidaiwa kuwa baadhi ya viongozi wa vyama hivyo wapo kwenye mjadala wa kushawishi wenzao kujiondoa kushiriki uchaguzi huo kama mambo hayatabadilika

Najuwa kuwa mamlaka zinazosimamia uchaguzi huo chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) zimejitokeza mara kadhaa kukanusha baadhi ya madai, lakini nadhani kelele zinapokuwa nyingi kila wakati ni wakati muafaka wa kuchukua hatua stahiki badala ya kudharau kabisa ili kulinda ustawi wa uchaguzi wenyewe na Taifa kwa ujumla wake

Hivi karibuni pia Jambo TV imefanya mahojiano na mwanaharakati Godlisten Malisa ambaye katika kuzungumzia sintofahamu hiyo alidai kuwa licha ya kwamba mambo yameharibika, lakini hapa tulipofikia na kwa siku zilizosalia kuelekea Novemba 27.2024 ambayo ni siku rasmi ya upigaji kura wahusika kwa maana ya serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Chama cha Mapinduzi (CCM) kama chama dola nchini na ofisi ya Rais-TAMISEMI inayo nafasi ya kufanya mabadiliko na mageuzi ili mambo yaende sawa na kuondoa malalamiko yanayojitokeza kwa kuwa hayana afya kwa mustakabali wa demokrasia na Taifa kwa ujumla wake.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!