Na Helena Magabe-Tarime
Umoja wa Wafanyabiashara Walemavu Tarime (UWAWATA) umeiomba jamii kuunga mkono juhudi zao za kujikwamua kiuchumi kupitia miradi ya kilimo, uuzaji wa nafaka na usagaji wa mazao, kwa lengo la kuondokana na utegemezi na hali ya kuombaomba.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa UWAWATA, Charles Bigoro Wambura, alisema kuwa walemavu si watu wasiokuwa na uwezo wa kufikiri, bali changamoto zao zipo kwenye viungo. Hivyo, wakiwezeshwa wanaweza kushiriki kikamilifu kwenye maendeleo ya taifa.
Amesema wameanzisha umoja huu ili kuungana, kushirikiana na jamii katika maendeleo. wailenga kujitegemea kwa kufanya biashara ya nafaka, kilimo, pamoja na kuwa na mashine ya kusaga na kukoboa.
Amebainisha kuwa wana mpango wa kuendesha harambee Julai 15, 2025, katika Hoteli ya CMG mjini Tarime, ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele. Lengo ni kupata mitaji kwa ajili ya miradi mitatu waliyoibuni:
- Duka la nafaka (thamani ya shilingi milioni 30)
- Mashine ya kusaga magunia 10 (thamani ya shilingi milioni 15)
- Mtaji wa kilimo (shilingi milioni 5)
Aidha, Wambura alisema kuwa licha ya kuwepo kwa mikopo ya asilimia 2 ya Halmashauri kwa walemavu, wengi wao hukwama kupata mkopo kutokana na masharti magumu, ikiwemo kutakiwa kuwa tayari na biashara inayoendelea.
Amesema wanakaribisha mtu yeyote anayeuguswa na jitihada zao. Hata kama hakualikwa rasmi kwa barua, anaweza kuja kuwaunga mkono siku hiyo.
Kwa upande wake, Mtunza Hazina wa Umoja huo, Esther Mongasyo Ikenga, alisema kuwa wamechoshwa na hali ya kuombaomba mitaani na wanataka kujitegemea kupitia miradi ya kiuchumi.
Mjumbe Christina Samson Marwa alisema kuwa utegemezi umekuwa chanzo cha kudharauliwa na jamii, lakini kupitia miradi yao, wanaamini watajenga heshima na maisha bora.
Esther Marwa Mantago, naye alisisitiza kuwa mtaji na msaada wa jamii ndio nguzo muhimu kwa wao kuondokana na dharau na unyanyapaa wanaopata kutokana na ulemavu wao.