Latest Posts

UTAFITI: WATOTO 53% CHINI YA MIAKA MITANO WAKABILIWA NA CHANGAMOTO ZA MAKUZI

Matokeo ya Utafiti wa Watu, Afya na Viashiria vya Malaria wa mwaka 2022 yanaonyesha kuwa asilimia 47 ya watoto wenye umri wa miezi 24 hadi 59 (chini ya miaka mitano) wako katika hatua za ukuaji timilifu, huku asilimia 53 wakibainika kuwa bado wanakumbwa na changamoto za makuzi, malezi na maendeleo ya awali ya mtoto.

Utafiti huo umetolewa  Jumatano, Julai 2, 2025 jijini Dodoma, wakati wa kikao kazi cha uwasilishaji wa viashiria vya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (ECDI 2030).

Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Prof. Tumaini Nagu, amesema tafiti hizo zinaonesha pia tofauti ya kijinsia kati ya watoto walioko kwenye ukuaji timilifu kati ya asilimia 47 ya watoto hao, asilimia 51 ni wasichana na asilimia 44 ni wavulana.

“Hili linaonyesha kwamba bado kuna haja kubwa ya kuwekeza katika malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa kuzingatia jinsia zote,” amesema Prof. Nagu.

Ameongeza kuwa asilimia 85 ya ukuaji wa ubongo wa mtoto hutokea katika siku 2,000 za mwanzo, hivyo hatua hiyo ni muhimu sana katika kuhakikisha usalama na ustawi wa mtoto na jamii kwa ujumla.

“Ni muhimu sote kuelewa kuwa masuala ya mtoto ni mtambuka na yanagusa sekta mbalimbali. Wadau wote wanapaswa kushiriki kwa kuzingatia taaluma zao ili kuhakikisha utekelezaji wenye ufanisi wa ajenda ya maendeleo ya awali ya mtoto,” amesisitiza.

Aidha, Prof. Nagu amesema kuwa matokeo ya utafiti huo yanaweka msingi madhubuti wa utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (TECDEN), Mwajuma  Kibwana, ameiomba Serikali na wadau wa maendeleo kuongeza juhudi katika kuboresha mazingira ya watoto ili kulijenga taifa lenye tija.

 

“Tunapozungumzia usawa wa kijinsia, hatuangalii mtu akiwa mtu mzima, tunaanza kumwangalia mtoto akiwa bado mdogo, tafiti hizi zinaonesha kuwa asilimia 30 ya watoto chini ya miaka mitano wanakabiliwa na changamoto kubwa, tunawajibika kuhakikisha kwamba watoto hawa wanapata uwekezaji unaostahili,” amesema  Kibwana.

Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha afya, ulinzi, usalama na fursa za ujifunzaji wa awali kwa watoto, sambamba na malezi yenye mwitikio wa karibu kutoka kwa wazazi na walezi.

“Bado tunakazi kubwa ya kufanya, lakini kwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau, tunaweza kuboresha hali hii na kufanikisha maendeleo ya watoto wetu kwa vizazi vijavyo,” amehitimisha.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!