Viongozi mbalimbali wa serikali wameombwa kuwasaidia Maafisa Elimu kwa kupita kwenye shule za msingi na sekondari ili kuongea na wanafunzi na kuwapa hamasa ya kufanya vizuri kwenye masomo na mitihani kwa ujumla.
Hayo ameyazungumza Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtwara Sisters iliyopo Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara Sister Stella Mnunduma,kwenye kikao kilichofanyika shuleni hapo kati ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Mwalimu Hassan Nyange na wanafunzi wa shule hiyo.
Sister Mnunduma amesema kuwa miaka ya nyuma hakukuwa na Mkurugenzi ambae alikuwa na destuli ya kuwatembelea wanafunzi na kuzungumza nao kuhusu taaluma,maisha,uzalendo na kuwatia moyo wa kusoma kwa bidii ili kukomboa mkoa na taifa la Tanzania ambapo viongozi mbalimbali wakipita.
Hivyo amewataka viongozi wengine kuiga mfano wa Mkurugenzi huyo kwani kufanya hivyo kunawatia moyo wanafunzi na walimu kwa ujumla kwa kujua kuwa hawako wenyewe kwenye kuhakikisha wanaongeza ufaulu wa Mkoa.
Kwa upande wa wanafunzi kutoka shule hiyo Anastazia Gervais na Mektridis Ndumbalo wamemshukuru Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Mwalimu Hassan Nyange kwa kuendelea kufatilia kwa ukaribu maendeleo ya wanafunzi hao pamoja na kisasa kuwasaidia bila kujali shule ya serikali au binafsi.
Sauda Issa na Fakihi Jafar Kutoka shule ya Call and Vision wameahidi kutomuangusha Mkurugenzi kwani amekuwa kiongozi anae pambana kwaajili ya kuwainua wanafunzi wenye changamoto mbalimbali ili kuhakikisha wanaendelea na masomo yao.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara Mwalimu Hassan Nyange amesema lengo la kuongea na wanafunzi mara kwa mara ni kuwakumbusha wanafunzi kuhusu nidhamu,taaluma na kuwaandaa na mitihani ya taifa ya kidato cha pili na cha nne pamoja na kuwaandaa kisaikolojia wanafunzi wa kidato cha sita kuhusu mitihani yao ya mwakani.
“Huu ni mwendelezo wa utamaduni wangu ambao ni wakawaida kabisa nikipita kwenye shule za msingi na sekondari kuhakikisha kwamba wanafunzi wa Mtwara Manispaa wanakuwa wanafunzi wa tofauti,tunawaandaa zaidi wanafunzi wetu kujiandaa kulisaidia taifa lao kuwa wazalendo,kuwa na nidhamu nzuri mashuleni na kuwa miongoni mwa watu watakao kuja kuwa na tija kwenye taifa hili.”Amesema Nyange
Mwalimu Hassan Nyange ametembelea shule mbili zilizopo Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara ambazo ni shule binafsi na kuwaahidi wanafunzi hao kuwasaidia vitabu ambavyo havipo kwenye shule hizo na vile vilivyokuwa vichache ambapo kila shule ameahidi kuwanunulia vitabu vya shilingi milioni 1.