Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara Mobutu Malima amemtaka Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mtwara mjini Salumu Naida kuhakikisha kasi ya kuongeza idadi ya wanachama inaongezeka ili kuwa na wanachama wengi.
Mobutu amesema hajaridhishwa na idadi ya wanachama wa CCM wilaya ya Mtwara mjini kwani wananchi waliopo kwenye wilaya hiyo ni zaidi ya milioni 1 lakini wanachama wa chama hicho ni elfu 43,000.
Hayo ameyaeleza kwenye ziara yake ya kujitambulisha katika manispaa hiyo
na kupata fursa ya kuzungumza na wanachama wa CCM kupitia mkutano wa ndani.
Amesema kusiwe na vikwazo na ubaguzi wa kuingiza wanachama wapya na kila mwanachama ana haki sawa na mwengine.
Pia amewataka wanachama hao kutumia vikao vya chama kwa ajili ya kuwasilisha changamoto zao na wananchi ila asiwepo mwanachama wa kuzungumza kero zake nje ya kikao kwani kufanya hivyo ni kukiaibisha chama.
“Tutumie vikao vya chama chetu kujua changamoto ya chama chetu,wanachama pamoja na wananchi wetu, lakini ndio sehemu ambayo tutakosoana kwa haki,staha,lugha nzuri na kuelezana ukweli lakini nje ya vikao likizungumzwa jambo hayo ni majungu.”Amesema Mobutu
Pia amemtaka Mwenyekiti huyo kusimama imara na kutokukubali kuwekwa mfukoni na kiongozi yoyote kwani yeye ni mwenyekiti wa taasisi na sio wa mtu binafsi na kusisitiza kuondoa makundi ya uchaguzi kwani yeye ndie anapaswa kuunganisha wanachama wote ili wawe wamoja.
Naye Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Mtwara, Juma Muruwa amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta vitendea kazi kwa watendaji wote wa kata ikiwa ni pikipiki na kuwaomba wahusika kwenda kufanyia kazi zilizokusudiwa.