Wananchi na wadau wa haki za watoto wamefanya matembezi ya amani siku ya Jumamosi ili kuonesha uchungu na huzuni yao juu ya ongezeko la matukio ya ukatili dhidi ya watoto nchini Tanzania.
Wakikusanyika kwa lengo la kuhamasisha hatua za haraka kulinda ustawi wa watoto, wadau hao wamesikitishwa na matukio ya hivi karibuni ya kubakwa, kulawitiwa, kutekwa, na hata mauaji ya watoto wadogo.
Ripoti za hivi karibuni zinathibitisha kuwa hali ya usalama wa watoto imezidi kudorora, ambapo mfano wa kusikitisha ni tukio la mtoto wa miezi sita kubakwa na kuuawa mkoani Dodoma.
Aidha, tukio jingine la mtoto wa miaka kumi na tatu aliyelawitiwa na kuuliwa pamoja na mama yake limeshangaza na kuibua hasira kutoka kwa wananchi. Matukio haya yanazidi kuongezeka huku uwajibikaji wa vyombo vya sheria ukielezwa kuwa hafifu katika kukamata, kupeleleza na kuwafikisha watuhumiwa mbele ya sheria.
Wananchi wamekumbusha kuwa takwimu zinaonesha ongezeko la asilimia 57 la matukio ya ulawiti, kutoka kesi 1,205 mwaka 2020 hadi 2,488 mwaka 2023. Hali kadhalika, matukio ya ubakaji yameongezeka kutoka 6,827 mwaka 2022 hadi 8,691 mwaka 2023. Wadau wameendelea kukemea matukio haya wakisema kuwa yanaathiri mustakabali wa taifa na kudhoofisha haki za watoto.
“Wakati huu ni muhimu kwetu sisi wananchi, wazazi, walezi, na walimu kuchukua hatua thabiti kulinda watoto wetu. Ulinzi wa watoto unahitaji ushirikiano wa jamii nzima, na hatuwezi kukaa kimya wakati mustakabali wa watoto wetu unahatarishwa na vitendo vya kinyama,” alisema mmoja wa watoa mada kwenye maandamano hayo.
Wananchi pia wametoa wito kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Jeshi la Polisi, kuongeza juhudi katika ufuatiliaji wa kesi hizi na kuhakikisha haki inatendeka haraka kwa waathirika wa matukio ya ukatili.