Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata kilogramu 1,815 za dawa za kulevya aina ya skanka katika operesheni iliyofanyika tarehe 28 Agosti, 2024 hadi tarehe 02 Septemba, 2024 katika maeneo ya Luguruni Mbezi na Magomeni jijini Dar es Salaam ambapo watuhumiwa watano (05) wamekamatwa kuhusiana na dawa hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar-es-salaam Kamishna Jenerali wa DCEA Tanzania Aretas Lyimo amesema watuhumiwa waliokamatwa wanatambulika kwa majina ya Richard Henry Mwanri (47) ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi Makonde wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na Felista Henry Mwanri (70) mkulima na mkazi wa Luguluni Mbezi Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam ambaye ni mmiliki wa nyumba zilipokutwa dawa hizo za kulevya.
Watuhumiwa wengine ni Athumani Koja Mohamed (58) mfanyabiashara, na mkazi wa Tanga, Omary Chande Mohamed (32) dereva bajaji na mkazi wa Buza jijini Dar es Salaam na Juma Abdallah Chapa (36) mkazi wa Kiwalani jijini Dar es Salaam.
Aidha, katika operesheni hiyo, gari aina ya Mitsubishi Pajero yenye namba za usajili T 551 CAB na bajaji yenye namba za usajili MC 844 CZV vimekamatwa
Richard Mwanri ni mhalifu ambaye amekuwa akipokea dawa za kulevya kutoka nchi mbalimbali na kuziingiza nchini kwa usafiri wa magari zikiwa zimefichwa kwa kuchanganywa na bidhaa nyingine kisha kusambazwa kwa wauzaji wengine katika maeneo mbalimbali nchini.