Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania Prof. Makame Mbarawa, ameiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha inasimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato pamoja na miradi inayotekelezwa chini ya mamlaka hiyo, ambayo serikali imewekeza fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi nchini.
Waziri Mbarawa ameyasema hayo wakati alipotembelea Bandari ya Ndumbi na Bandari ya Mbambabay, ambayo ipo kwenye hatua za awali za ujenzi. Mradi huo unatarajiwa kugharimu Shilingi bilioni 75.84 hadi kukamilika kwake.
Katika ziara yake, Waziri Mbarawa amesisitiza kuwa serikali ya awamu ya sita imewekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye ujenzi wa bandari nchini, hivyo ni muhimu kwa TPA kusimamia miradi hiyo kwa ufanisi mkubwa na kuhakikisha mapato yanakusanywa kikamilifu.
![](https://jambo.co.tz/wp-content/uploads/2024/09/WhatsApp-Image-2024-09-19-at-12.19.26.jpeg)
“Wenye jukumu la kusisimia mradi ni sisi serikali yaani wizara pamoja na TPA, kazi yangu ni kuwaambia TPA wasiamamie mradi huu kwa uadilifu mkubwa, TPA tujipange tuhakikishe kwamba Bandarini hasa Dar es Salaam na maeneo mengine hakuna upotevu wowote wa fedha, upotevu wa fedha maana yake unachelewesha utekeleaji wa miradi yetu” amesema Mbarawa
Pia ameeleza kuwa kukusanya mapato kwa ufanisi kutasaidia kuleta matokeo chanya katika sekta ya uchukuzi, hususan katika uendelezaji wa miradi ya bandari na miundombinu.
“Tunasimamia ukusanyaji wa mapato, kwani bila mapato haya, hatuwezi kutekeleza miradi. Bunge lililopita lilipitisha ombi la kupewa wafredge kwa ajili ya kuendeleza miundombinu, hivyo ni muhimu kuhakikisha mapato haya yanakusanywa kwa ufanisi ili kuendelea na miradi hii”, amesema.
![](https://jambo.co.tz/wp-content/uploads/2024/09/WhatsApp-Image-2024-09-19-at-12.17.19.jpeg)
Waziri Mbarawa pia amezungumzia umuhimu wa ujenzi wa Bandari ya Mbambabay, akisema kuwa itasaidia kufungua fursa za kiuchumi katika maeneo yaliyo jirani na Ziwa Nyasa, hususani kwa kurahisisha shughuli za kibiashara kati ya Tanzania na nchi jirani kama Malawi. Amesisitiza kuwa bandari hiyo itajengwa kwa muda uliopangwa ili kufikia malengo ya kiuchumi kwa taifa na nchi jirani.
Kwa upande wake, Mbunge wa Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya, ametoa pongezi kwa juhudi za serikali katika ujenzi wa bandari hiyo, akibainisha kuwa itakuwa muhimu kwa uchumi wa wilaya ya Nyasa. Amesema bandari hiyo ni moyo wa uchumi wa wananchi wa eneo hilo, kwani itawawezesha kufanya biashara na kuimarisha uchumi wa familia zao.
“Bandari ya Mbambabay ni tegemeo kubwa kwa wananchi wa maeneo haya, hasa kwa biashara za kahawa na mihogo, na itatuwezesha kufanya biashara na nchi jirani kama Malawi,” amesema Mhandisi Manyanya.
Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Juma Kijavara, amesema kuwa mradi wa ujenzi wa Bandari ya Mbambabay umeshatekelezwa kwa asilimia 6. Mradi huo utahusisha ujenzi wa gati, sehemu za kuhifadhia mizigo ndani na nje, nyumba za wafanyakazi, pamoja na ujenzi wa barabara ya mita 750 itakayounganisha bandari hiyo na Wilaya ya Mbinga.
![](https://jambo.co.tz/wp-content/uploads/2024/09/WhatsApp-Image-2024-09-19-at-12.17.13.jpeg)
Amefafanua kuwa barabara ya Mbinga hadi Mbambabay, yenye urefu wa kilomita 66, itajengwa na kuunganishwa na bandari hiyo.
Mradi wa ujenzi wa bandari hiyo unaotekelezwa na mkandarasi kutoka China, kampuni ya Sheman-Ongoing Constraction Company, kwa kushirikiana na kampuni ya Anova, unatarajiwa kugharimu takriban Shilingi bilioni 75.84 hadi kukamilika kwake ndani ya miezi 24.