Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amemwagiza Kamishna Mkuu mpya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Juma Mwenda kuwachukulia hatua kali za kisheria na kinidhamu ikiwamo kuwafukuza kazi baadhi ya watumishi wa mamlaka hiyo wanaokiuka maadili ya kazi zao kama kudai na kupokea rushwa, kwa kuwa vitendo hivyo vinaitia doa TRA na kuikosesha Serikali mapato.
Dkt. Nchemba amesema hayo wakati akihitimisha Kikao cha Tathmini ya Utendaji Kazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 kilichofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC).
Aidha Dkt. Nchemba amemwagiza Kamishna huyo kuwachukulia hatua kali wafanyabiashara wasiowasilisha ritani za Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa kuwa fedha hizo zinatakiwa kuwasilishwa serikalini kupitia TRA ikizingatiwa kuwa wafanyabiashara ni Mawakala wa Serikali wa kukusanya kodi hiyo, na hazitakiwi kufanywa kama sehemu ya mapato yao.
Halikadhalika Dkt. Nchemba amewataka watumishi wa TRA kuongeza ubunifu, umahiri na kuhakikisha wanatenda haki wakati wa kukusanya mapato ya Serikali ili kutimiza matarajio ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwaletea Watanzania maendeleo ya uhakika.
Pia Dkt. Nchemba ametumia fursa hiyo kuwapongeza TRA kwa utendaji kazi mahiri kwa mwaka wa fedha ulioisha wa 2023/24, ambapo walikusanya kiasi cha Shilingi trilioni 27.64, ambayo ni sawa na ufanisi wa asilimia 97.67 ya lengo la kukusanya Shilingi trilioni 28.30 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 14.50, ikilinganishwa na makusanyo ya Shilingi trilioni 24.14 katika mwaka wa fedha uliopita 2022/23.
Katika hafla hiyo Dkt. Nchemba aliambatana na Naibu Waziri wa Fedha Hamad Hassan Chande, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Sera Wizara ya Fedha William Mhoja, na maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha.