Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Morogoro limekutana na wadau wa nishati kwa ajili ya kutafuta suluhu ya kudumu katika kukabiliana na ongezeko la matukio ya wizi wa vyuma vinavyomilikiwa na Shirika hilo ambavyo ni sehemu ya miundombinu muhimu ya usambazaji Umeme.
Wizi wa vifaa vya shirika hilo vya kuchakata na kusambaza umeme unalipelekea Shirika kupata hasara, ikiwemo kupoteza Mabilioni ya fedha kutokana na kuchukua hatua za kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa huku ikihatarisha usalama wa wananchi katika kuathiri hali ya upatikanaji wa huduma za umeme.
Akizungumza katika kikao hicho, Afisa Usalama wa TANESCO mkoa wa Morogoro, Chroloquine John amesema lengo la kikao hicho ni kuweka mikakati madhubuti ya kulinda miundombinu ya Serikali ili kuzuia uharibifu unaoendelea kufanyika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa EWURA (CCC) mkoa wa Morogoro, Potamia Burreta, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha taarifa za taka hatarishi zinazoletwa zinathibitishwa uhalali wake kabla ya kuuzwa au kununuliwa.
Naye, Katibu wa wauza taka hatarishi Morogoro, Mussa Ally ameeleza vitendo hivyo vinatekelezwa na wananchi wasio waaminifu hasa wauzaji wa taka hatarishi ambao hujihusisha na ununuzi na uuzaji wa vifaa hivyo bila kuzingatia vyanzo vyake.