Hatua ya kampuni ya Amson Group ya Tanzania kuinunua kampuni ya saruji ya nchini Kenya ya Bamburi Cement kwa Dola milioni 180 (takriban Shilingi za Kitanzania bilioni 475) imeungwa mkono na wamiliki wakuu wa hisa wa Bamburi.
Kampuni ya Amsons ilitangaza nia yake ya kuinunua Bamburi Cement mapema mwezi uliopita katika hatua ambayo ikikamilika, itaweka historia ya kuwa mojawapo ya mikataba mikubwa zaidi ya ununuzi wa kampuni Afrika Mashariki na kutengeneza mzalishaji mkubwa wa saruji katika eneo hilo.
Amsons Group ambayo ni biashara ya familia inayofanya shughuli zake nchini Tanzania, Zambia, Malawi, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi ilisema Jumatano kwamba imetia saini ofa ya kisheria na Bamburi Cement.
Mkataba huo utakuwa uwekezaji mkubwa zaidi wa kibinafsi wa kampuni ya Kitanzania nchini Kenya tangu kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mnamo 1977, ukiushinda uwekezaji wa dola milioni 130 wa kampuni nyingine kutoka Tanzania ya Taifa Gas inayomilikiwa na tajiri wa Kitanzania Rostam Aziz, ambayo kituo chake cha uzalishaji wa gesi za kupikia (LPG) kilizinduliwa Kenya Februari 2023.
Katika uwekezaji huo, zabuni ya Amsons Group imepata kuungwa mkono na wanahisa wakuu wa Bamburi Cement ikiwamo Holcim ambayo ni kampuni ya kimataifa yenye makao yake makuu nchini Uswizi.
Holcim inayojishughulisha na vifaa vya ujenzi imekubali kuuza hisa zake zote za Bamburi kwa Amsons, kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni ya Bamburi Cement kama ilivyoripotiwa na Kituo cha habari cha Standard Media cha Kenya.
Holcim inamiliki asilimia 58.6 ya jumla ya mtaji wa hisa wa Bamburi kupitia kampuni za Fincem Holding (asilimia 29.3) na Kencem Holding (asilimia 29.3). Taasisi za Kenya na watu binafsi wanamiliki wastani wa asilimia 32.17 ya hisa za Bamburi huku asilimia nyingine 9.23 ikimilikiwa na wawekezaji wengine wa kigeni.
“Amsons imethibitisha kuwa mnamo Julai 10, 2024, ilipokea ahadi isiyoweza kubatilishwa kutoka kwa wanahisa wafuatao wa Bamburi kama sehemu ya ofa: Fincem Holdingna Kencem Holding”, ilieleza taarifa ya Bamburi Cement.
Kulingana na taarifa hiyo ambayo Standard Media ilinukuu, kampuni ya Bamburi Cement ilisema imepata uthibitisho kwamba Amsons walikuwa na uwezo wa kupata fedha za kutosha kukamilisha mpango huo.
“Kulingana na taarifa ya mtoa ofa, KCB Investment Bank Ltd ikiwa ni mshauri wa miamala na dalali mfadhili wa Amsons, imethibitisha kuwa Amsons ina rasilimali za kutosha za kifedha ili kukidhi malipo ya hisa zote za Bamburi”, ilieleza Bamburi.
Hata hivyo muamala na ununuzi wa ujumla unategemea idhini za udhibiti.
“Iwapo ofa itafikia asilimia 75 au zaidi ya hisa za ofa, mtoa ofa atatathmini ufanisi wa Bamburi kubaki kwenye soko la hisa na baada ya hapo kwa kutegemea idhini ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji (CMA), ataomba Bamburi ifutwe kutoka NSE (Soko la Hisa la Nairobi)”, ilisema taarifa ya Bamburi kama ilivyonukuliwa na Standard Media.
Mkurugenzi Mtendaji wa Amsons Group, Edha Nahdi alisema mwezi uliopita kuwa mkataba uliopendekezwa utaongeza wigo nafasi ya kundi hilo katika sekta ya saruji Afrika Mashariki kama sehemu ya maendeleo ya uchumi wa kanda na malengo ya ushirikiano wa masoko.
“Tuna mipango mizuri ya kuimarisha uwekezaji wetu nchini Kenya kupitia Bamburi. Ofa yetu ya kupata hisa Bamburi ni sehemu ya mpango wetu wa upanuzi wa soko la kampuni na itaashiria kuingia rasmi kwa Amsons Group katika soko la Kenya ambapo tunapanga kufanya uwekezaji katika viwanda vingine katika miezi ijayo”, ameeleza Nahdi.
Amsons Group ilianzishwa mwaka 2006 nchini Tanzania na sasa ina zaidi ya dola bilioni 1 katika mauzo ya kila mwaka.
Shughuli zake kuu za biashara kihistoria zilihusisha uagizaji wa mafuta kwa wingi na bidhaa za petroli chini ya chapa ya rejareja ya Camel Oil Tanzania.
Kwa muda sasa, Amsons imeendelea kukuza wigo wake katika sekta ya viwanda ikitengeneza saruji tani 6,000 kwa siku ambazo zimetengenezwa pia kupitia kituo cha saruji cha Mbeya ilichokinunua hivi karibuni.