Wazazi na walezi wametakiwa kujenga mahusiano mazuri na watoto wao ili waweze kupokea taarifa muhimu kuhusu matukio wanayokutana nayo, hususan matukio ya kikatili dhidi yao.
Tunda Stambuli, Mjumbe wa Jukwaa la Wanawake Mtwara akizungumza kwenye mafunzo ya mradi wa Sauti Zetu Project ulioandaliwa na jukwaa hilo amesema kwamba kuna watoto wengi wanaogopa wazazi wao, hali inayosababisha watoto kupitia ukatili na kunyamaza kimya kwa kuhofia kupokea adhabu kutoka kwa wazazi wao.

“Tunahitaji kuwa karibu na watoto na kutoa elimu inayowasaidia wazazi kuwa na muda wa kutosha na watoto wao. Watoto mara nyingi wanaogopa wazazi wao, na kesi nyingi tunazipokea,” amesema Tunda.
Ameongeza kuwa, “Wakati mzazi anakuwepo, mtoto mara nyingi ana hofu na hatasema chochote, lakini ikiwa mzazi hayupo, mtoto anaweza kufunguka na kusema kweli. Vitendo vya ukatili vinaanzia mara nyingi ndani ya familia.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Mariamu Chimbwai, amesema kwamba kwa muda mrefu elimu ya kukomesha ukatili imekuwa ikielekezwa kwa wanawake pekee, hali ambayo imepelekea kuibuka kwa changamoto kubwa ya watoto wa kiume kulawitiwa. Hivyo, wameona umuhimu wa kupaza sauti juu ya kukomesha matukio haya ya ulawiti.
Sambamba na hilo, amewataka wanawake kuacha kujibweteka na badala yake wajishughulishe ili waweze kujiingizia kipato na kuacha kutegemea wanaume, ambao baadhi yao wanakumbana na ukatili wa kuingiliwa kinyume na maumbile kutokana na kuwa tegemezi.
Akitoa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia, Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Fatuisa Mapua, amesema kwamba wazazi wengi ni chanzo cha kukatisha mnyororo wa haki jinai kutokana na kutotoa ushirikiano kwenye mamlaka husika.
“Katika kesi nyingi, ushahidi umeharibika kwa sababu wazazi wanashindwa kutoa ushahidi wao kwa wakati. Wazazi tunapaswa kuwa mstari wa mbele katika kupigania haki za watoto kwa maslahi mapana ya baadaye,” amesema Mapua.