





Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu
Tanzania (TEA), Dkt. Erasmus Kipesha, leo Februari 11, 2026 amewasilisha taarifa kuhusu majukumu na utendaji wa mamlaka hiyo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo.
Wasilisho hilo limefanyika katika muktadha wa mafunzo yaliyotolewa kwa wajumbe wa kamati hiyo, yakilenga kuwajengea uelewa wa kina kuhusu majukumu, muundo na utendaji wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Dkt. Kipesha ameeleza majukumu ya TEA, hususan katika usimamizi na uendeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Elimu, akifafanua namna mfuko huo unavyotekeleza miradi ya maendeleo ya sekta ya elimu nchini.
Aidha, wajumbe wa kamati walipata fursa ya kuuliza maswali na kupatiwa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo, ikiwemo vigezo vya upangaji na ufuatiliaji wa miradi inayogharimiwa kupitia mfuko huo.
Kwa mujibu wa Dkt. Kipesha, katika kipindi cha miaka kumi kuanzia mwaka wa fedha 2015/2016 hadi 2025/2026, jumla ya miradi 1,711 yenye thamani ya shilingi bilioni 128.5 imetekelezwa kupitia Mfuko wa Taifa wa Elimu.
Amesisitiza kuwa TEA itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha uwazi, uwajibikaji na thamani ya fedha katika kuimarisha miundombinu na huduma za elimu nchini.