Latest Posts

MFUMO WA TANOGA KUIMARISHA UDHIBITI WA MIZIGO NA MAPAMBANO DHIDI YA BIDHAA FEKI

Mfumo wa kidijitali wa TANOGA (Tanzania Other Government Agencies) umetajwa kuwa chombo muhimu katika kuimarisha udhibiti wa mizigo inayoingia nchini na kupambana na bidhaa feki, kwa kuwezesha taasisi za serikali kuratibu utoaji wa vibali na ukaguzi kwa wakati mmoja.

Akizungumza katika semina ya siku moja kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari iliyoandaliwa na Tume ya Ushindani (FCC) jijini Dar es Salaam Februari 23, 2026 , Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Khadija Ngasongwa, amesema TANOGA ni jukwaa la mtandao linalounganishwa na mfumo wa forodha wa Tanzania.

Amesema mfumo huo unafanya kazi kwa mtindo wa Dirisha Moja la kutolea huduma zote (single window system), ambapo vyombo vyote vya udhibiti na ukaguzi hupata taarifa za mizigo kwa wakati mmoja, hatua inayorahisisha usimamizi na kuongeza uwazi.

“Lengo ni kutrack na kutrace chanzo cha bidhaa zinazoingia nchini. Kupitia TANOGA tunaweza kubaini bidhaa imezalishwa wapi, nani mhusika wake, na kama ni halali au imeghushiwa,” alisema Ngasongwa.

Kwa mujibu wake, TANOGA ni sehemu ya miundombinu ya kidijitali ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na ulianza kutumika Desemba mwaka jana, ukiwa na dhima ya kurekodi na kuratibu uingizaji wa bidhaa (importation of goods) pamoja na kurahisisha mawasiliano kati ya taasisi za udhibiti.

Ameongeza kuwa kupitia mfumo huo, FCC inashirikiana na taasisi mbalimbali za serikali zikiwemo Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ili kuhakikisha bidhaa zinazoingia sokoni zinakidhi viwango na sheria zilizopo.

Akifungua semina hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali kama TANOGA ni hatua muhimu katika kulinda uchumi wa taifa.

Amesema udhibiti madhubuti wa bidhaa feki ni sehemu ya kulinda soko la ndani na watumiaji, akionya kuwa bila mifumo thabiti ya usimamizi, nchi inaweza kuwa soko la bidhaa zisizo na ubora.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bakari Kimwaga, amesema vyombo vya habari vina wajibu wa kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa mifumo ya udhibiti wa bidhaa na sheria za ushindani.

Semina hiyo ya siku moja kwa ilikuwa sehemu ya mkakati wa FCC wa kuimarisha ushirikiano na wadau wa habari, kwa lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusu sheria za ushindani na mapambano dhidi ya bidhaa bandia nchini.

Mfumo wa TANOGA (Tanzania Other Government Agencies) ni mfumo wa kielektroniki wa ushirikiano unaotumiwa na Tume ya Ushindani (FCC) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kurahisisha ukaguzi wa bidhaa zinazoingia nchini, huku lengo kuu likiwa ni Kurahisisha ukaguzi wa bidhaa bandia na kuhakikisha usalama wa walaji kwa kukagua bidhaa kwa pamoja na taasisi nyingine za udhibiti

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!