Latest Posts

ZAMBIA NA TANZANIA ZAKUBALI KUSHUSHA MAFUTA KWA DIPSTICK

Chama cha Wafanyakazi wa Malori Tanzania (CHAWAMATA) kimesema hatua ya Serikali ya Zambia kuruhusu matumizi ya kipimo cha dipstick katika ushushaji wa mafuta ni ushindi mkubwa kwa madereva wa malori ya matanki ya mafuta.

Kupitia makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Zambia pamoja na wakala wa vipimo wa pande zote mbili, hati ya makubaliano ilisainiwa Desemba 10, 2025, kuruhusu rasmi matumizi ya vipimo vya dipstick na chart badala ya mfumo wa awali wa floor meter.

Kwa mujibu wa chama hicho, mfumo wa awali wa floor meter ulikuwa ukisababisha tofauti za vipimo na kuzalisha mianya ya upotevu wa mafuta, hali iliyokuwa ikiwaweka madereva katika tuhuma za “shoti”. Mara nyingi madereva walilazimika kufidia hasara kwa fedha zao binafsi kulingana na bei ya mafuta ya siku husika, jambo lililosababisha madhara makubwa ya kiuchumi na kisaikolojia.

Akizungumza Februari 25, 2026, Katibu Mkuu wa chama hicho, Michael Greyson, amesema mafanikio hayo yamepatikana baada ya mchakato mrefu wa mazungumzo na vikao vya kitaalamu vilivyoanza tangu mwaka 2018.

Amesema changamoto ya shoti haikuishia kwenye hasara ya fedha pekee, bali ilisababisha baadhi ya madereva kupoteza mali, kufungwa, na wengine kupata madhara ya kiafya kutokana na msongo wa mawazo. Kutokana na hali hiyo, chama kiliandaa na kuwasilisha ripoti maalum serikalini ikieleza madhara ya mfumo uliokuwa unatumika.

Serikali ya Zambia tayari imetangaza kuanza rasmi kushusha mafuta kwa kutumia kipimo cha dipstick kinachotolewa Tanzania, hatua inayotarajiwa kuondoa malalamiko ya muda mrefu ya madereva.

Hata hivyo, chama hicho kimesema bado kuna masuala mengine yanayohitaji ufumbuzi, ikiwemo changamoto za mikataba, malipo ya risk allowance na maslahi mengine ya kazi. Hoja hizo tayari zimewasilishwa serikalini na zinasubiri kufanyiwa kazi.

Madereva wametakiwa kuendelea kuwa watulivu wakati serikali ikiendelea kushughulikia changamoto zilizosalia, huku chama kikisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa salama, ya haki na yenye kulinda maslahi ya madereva wote.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!