Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetangaza kuifuta usajili wake mara moja meli ya EAGLE (IMO No. 8203074) kufuatia taarifa za kukamatwa kwa chombo hicho nchini El Salvador kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya.
Kulingana na taarifa iliyotolewa leo Februari 27, 2026 na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar, meli hiyo inadaiwa kuwa ilikuwa inapeperusha bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Usajili wa Meli za Kimataifa wa Zanzibar (TZIRS). Taarifa za kukamatwa kwake ziliibuka Februari 17, 2026, kupitia mamlaka za Jamhuri ya El Salvador na vyombo vya habari vya kimataifa.
Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), ikitekeleza wajibu wake kama Dola ya Bendera (Flag State), imechukua hatua zifuatazo tangu Februari 18, 2026: kufuta usajili wa meli ya EAGLE ambapo imeondolewa rasmi kwenye rejista ya meli za Zanzibar, serikali imewasiliana na Jeshi la Polisi la Kimataifa (INTERPOL) kwa ajili ya uthibitisho wa kina na ushirikiano wa kiuchunguzi, na kuanzisha uchunguzi wa kisheria dhidi ya wahusika kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Usafiri Baharini Zanzibar.
“Pamoja na hayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina sera ya kutovumilia kabisa matumizi mabaya ya Bendera yake kwa shughuli zozote za uhalifu wa kimataifa, ikiwemo: usafirishaji wa dawa za kulevya, biashara haramu ya binadamu, uvunjifu wa vikwazo vya kimataifa na uhalifu wa kifedha au wa kimazingira baharini”, imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa iwapo tuhuma hizi zitathibitishwa, uwajibikaji utakuwa wa watu binafsi au wamiliki wa chombo husika, na si wa Mamlaka ya Bendera, kwa mujibu wa misingi ya sheria za kimataifa.
Hata hivyo, Serikali imeeleza utayari wake wa kushirikiana na Jamhuri ya El Salvador kupitia njia rasmi za kidiplomasia ili kupata ukweli wote wa tukio hilo. SMZ imehakikishia jumuiya ya kimataifa kuwa TZIRS inaendeshwa kwa taratibu madhubuti za uhakiki wa wamiliki halisi wa vyombo (beneficial ownership verification) na ufuatiliaji wa utiifu wa sheria za kimataifa (UNCLOS, SOLAS, na MARPOL).
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesisitiza kuwa inasimamia kwa umakini na weledi mkubwa Usajili wake wa Kimataifa wa Meli na itaendelea kuchukua hatua kali, za haraka na za kisheria pale ambapo ukiukwaji wowote utakapothibitishwa.