

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeialika sekta binafsi kuwekeza katika miradi midogo ya kuzalisha umeme vijijini, ikisema iko tayari kuwezesha wawekezaji wenye maeneo yenye vyanzo vya maji ili kuongeza uzalishaji wa nishati katika gridi ya taifa.
Wito huo umetolewa leo Jumatano Machi 11, 2026 wakati wa ziara ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) lililotembelea mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Lupali wenye uwezo wa kuzalisha kilowati 317 unaotekelezwa katika Kijiji cha Boimanda, Kata ya Matola, Wilaya ya Njombe mkoani Njombe.
Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji wa Miradi kutoka REA, Mhandisi Emmanuel Yessaya, amesema miradi ya uzalishaji umeme inayotekelezwa na sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika nchini.
Amesema Serikali kupitia REA inaendelea kusaidia wawekezaji wa sekta binafsi kwa kuwa ni wadau muhimu katika kukuza sekta ya nishati na maendeleo ya uchumi.
“Tunatoa wito kwa wawekezaji kutumia fursa ya vyanzo vya maji vilivyopo katika maeneo mbalimbali, hususan mikoa ya Njombe, Iringa na Ruvuma, kuwekeza katika miradi ya kuzalisha umeme ili kusaidia kuongeza nishati katika gridi ya taifa,” alisema Yessaya.
Kwa mujibu wa Yessaya, Serikali kupitia REA imetoa ruzuku ya shilingi bilioni 5.4 kufanikisha utekelezaji wa mradi wa Lupali kuanzia hatua za maandalizi hadi ujenzi wake.
Ameongeza kwa kusema kuwa, hadi sasa ujenzi wa miundombinu ya mradi huo umekamilika na kilichobaki ni kuwasha mtambo pamoja na kuunganisha umeme katika gridi ya taifa, hatua itakayoongeza kilowati 317 katika mfumo wa umeme wa taifa kupitia Mkoa wa Njombe.
Mradi huo unatekelezwa na Shirika la Benedictine Sisters of St. Gertrud Convent Imiliwaha na unatumia maporomoko ya maji katika mto unaopita katika Kijiji cha Boimanda kuzalisha umeme.
Awali, mradi huo ulianzishwa kwa lengo la kuzalisha umeme kwa matumizi ya taasisi za shirika hilo ikiwemo hospitali, shule, karakana na gereji, lakini baadaye ulipanuliwa ili kunufaisha jamii kwa kuunganisha vijiji vitatu vya Matola, Boimanda na Kitulila.
Mratibu wa Mradi huo,
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa kuzalisha umeme wa Lupali, Sister Imaculatha Mlowe, amesema Serikali kupitia REA imechangia kwa kiasi kikubwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi.
Amesema mchango huo umehusisha kugharamia tafiti za awali za mradi, ujenzi wa njia kuu za kusafirisha umeme za msongo wa kilovoti 11 zenye urefu wa kilomita 23.48 pamoja na njia ndogo za kusambaza umeme kwa watumiaji zenye urefu wa kilomita 30.61.
Pia amesema ruzuku hiyo
imewezesha kukamilika kwa miundombinu muhimu ya mradi ikiwemo ujenzi wa intake weir, jengo la kuzalishia umeme (power house) na uwekaji wa mabomba ya kusafirisha maji (penstock).
Kwa mujibu wa Mlowe, miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme kwa watumiaji imekamilika na kutokana na gridi ya taifa kufika katika kijiji jirani cha Kitulila, mawasiliano yalifanyika kati ya TANESCO na shirika hilo ili wananchi waanze kupata huduma ya umeme kupitia miundombinu ya mradi wakati ukamilishaji wa ujenzi ukiendelea.
Kadhaalika amebainisha kuwa, TANESCO tayari iliunganisha umeme katika Kijiji cha Boimanda na kuanza kutoa huduma kwa wananchi tangu Februari 2023.
Kwa sasa zaidi ya wananchi 212 wa Kijiji cha Boimanda wanapata huduma ya umeme kupitia gridi ya TANESCO, huku wananchi 366 wa Kijiji cha Matola wakipata umeme kupitia mradi wa zamani wa Lupali.
Mlowe amesema, mkataba wa kuuza umeme kati ya TANESCO na Shirika la St. Benedictine of Imiliwaha tayari umeshasainiwa na kazi za mwisho za kukamilisha mradi zinatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu ijayo.
Akiainisha faida zake amesema mradi huo unatarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi katika eneo hilo, ikiwemo uanzishwaji wa biashara na viwanda vidogo kama kusindika nafaka, useremala, uchomeleaji vyuma na ushonaji.
Aidha, amesema mradi huo utasaidia kuboresha utoaji wa huduma katika taasisi mbalimbali kama shule, zahanati na vituo vya afya pamoja na kupunguza matumizi ya nishati zisizo rafiki kwa mazingira kama mafuta ya taa, kuni na mkaa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amewataka Watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji katika uzalishaji wa umeme vijijini kwa kutumia vyanzo vya maji vinavyopatikana katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema miradi ya uzalishaji umeme ni muhimu katika kukuza uchumi wa taifa na itasaidia Tanzania kufikia malengo ya kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka megawati 4,031 za sasa hadi kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.