Latest Posts

MRADI WA UMEME LUPALI KUONGEZA KILOWATI 317 KWENYE GRIDI YA TAIFA

 

 

 

Mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Lupali wenye uwezo wa kuzalisha kilowati 317 unaotekelezwa katika Kijiji cha Boimanda, Kata ya Matola, Wilaya ya Njombe mkoani Njombe unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu ijayo na kuongeza uzalishaji wa umeme katika gridi ya taifa.

 

Mradi huo unaotekelezwa na Shirika la Benedictine Sisters of St. Gertrud Convent Imiliwaha umepata ruzuku ya Sh bilioni 5.4 kutoka Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ili kufanikisha utekelezaji wake kuanzia hatua za maandalizi hadi ujenzi.

 

Akizungumza wakati wa ziara ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) lililotembelea mradi huo leo Jumatano Machi 11, 2026 Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji wa Miradi wa REA, Mhandisi Emmanuel Yessaya amesema miundombinu ya mradi huo imekamilika na kilichobaki ni kuwasha mtambo na kuunganisha umeme katika gridi ya taifa.

 

Amesema mradi huo ni sehemu ya uwekezaji wa sekta binafsi katika uzalishaji wa umeme ambao utaingizwa kwenye gridi ya taifa kupitia Mkoa wa Njombe.

 

“REA tunaendelea kusaidia sekta binafsi kwa kuwa ni chachu ya maendeleo ya nchi yetu. Miradi kama hii inasaidia kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi na kuchochea shughuli za kiuchumi,” alisema Yessaya.

 

Sambamba na hayo, ametoa wito kwa wawekezaji kutumia fursa zilizopo katika maeneo yenye vyanzo vya maji hususan katika mikoa ya Njombe, Iringa na Ruvuma kuwekeza katika miradi ya kuzalisha umeme ili kusaidia kuongeza nishati katika gridi ya taifa.

 

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi huo, Sister Imaculatha Mlowe amesema Serikali kupitia REA imechangia kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa mradi huo.

 

Amesema mchango huo unahusisha kugharamia tafiti za awali za mradi, ujenzi wa njia kuu za kusafirisha umeme za msongo wa kilovoti 11 zenye urefu wa kilomita 23.48 pamoja na njia ndogo za kusambaza umeme kwa watumiaji zenye urefu wa kilomita 30.61.

 

Ameongeza kuwa ruzuku hiyo pia ilisaidia kukamilisha miundombinu ya mradi ikiwemo ujenzi wa intake weir, jengo la kuzalishia umeme (power house), uwekaji wa mabomba ya kusafirisha maji (penstock) pamoja na kazi nyingine za ujenzi.

 

Ameendelea kwa kusema kuwa, miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme imeshakamilika na gridi ya taifa kupitia TANESCO tayari imefika katika kijiji jirani cha Kitulila ambapo pia mawasiliano yalifanyika kati ya TANESCO na shirika hilo ili wananchi waanze kupata huduma ya umeme kupitia miundombinu ya mradi wakati ukamilishaji wa ujenzi ukiendelea.

 

“TANESCO tayari iliunganisha umeme katika kijiji cha Boimanda na kuanza kutoa huduma kwa wananchi tangu Februari 2023,” alisema Mlowe.

 

Amesema hadi sasa zaidi ya wananchi 212 wa Kijiji cha Boimanda wameunganishwa na kupata huduma ya umeme kupitia gridi ya TANESCO, huku wananchi 366 wa Kijiji cha Matola wakipata umeme kupitia mradi wa zamani wa Lupali.

 

 

Akizungumzia faida za mradi huo, amesema utahakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa matumizi ya nyumbani, biashara na taasisi mbalimbali ikiwemo shule, hospitali na karakana.

Aidha, amesema mradi huo utachochea uanzishwaji wa biashara na viwanda vidogo kama kusindika nafaka, useremala, uchomeleaji vyuma na ushonaji, hatua itakayosaidia kuongeza kipato cha wananchi na kukuza uchumi wa eneo husika.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amewapongeza Masista wa Shirika la St. Benedictine of Imiliwaha kwa kuanzisha mradi huo ambao ulilenga kutatua changamoto ya upatikanaji wa umeme katika vijiji vya Matola, Boimanda na Kitulila.

 

Balile ameongeza kwa kusema kuwa, mradi huo unaonesha namna ambavyo ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi unavyoweza kusaidia kuharakisha maendeleo ya kiuchumi nchini.

 

Vilevile ameeleza kuwa uzalishaji wa umeme ni moja ya vigezo muhimu vya maendeleo ya taifa na kwamba miradi kama hiyo itasaidia Tanzania kufikia malengo ya kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka megawati 4,031 za sasa hadi kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.

Katika hatua nyingine, amewataka Watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji katika uzalishaji wa umeme zinazotolewa na REA, akisisitiza kuwa taasisi hiyo iko tayari kusaidia wawekezaji wenye maeneo yenye vyanzo vya maji vinavyoweza kutumika kuzalisha umeme.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!