Latest Posts

MADUARA MANNE YAPOROMOKA MGODI WA MSASA, YAELEZWA HAKUNA MADHARA KWA BINADAMU

Na Joel Maduka, Geita

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, kwa kushirikiana na Kaimu Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa huo, ASF Keneth Mwakasitu, wamefuatilia kwa karibu zoezi la uokoaji kufuatia kuporomoka kwa maduara manne katika Mgodi wa Dhahabu wa Msasa uliopo wilayani Bukombe.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio, SACP Safia Jongo amesema kuwa ajali hiyo haijasababisha madhara yoyote kwa binadamu.

“Hakuna madhara kwa binadamu yaliyotokana na tukio hili. Tumeendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika eneo husika ili kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao,” amesema Jongo.

Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, ASF Keneth Mwakasitu, amesema zoezi la utafutaji linaendelea kwa kushirikiana na wananchi.

“Tunaendelea na zoezi la utafutaji kwa weledi mkubwa kwa kushirikiana na wananchi, na tayari baadhi ya vifaa vilivyokuwa vinatumika katika uchimbaji vimepatikana,” amesema Mwakasitu.

Naye Chifu Mkuu wa Mgodi wa Msasa, James Nkamba, amesema zoezi hilo linaendelea vizuri huku jitihada zikielekezwa katika kuhakikisha mali zote zilizofukiwa zinapatikana.

“Tunafanya kila juhudi kuhakikisha mali zote zilizofukiwa zinapatikana, sambamba na kuimarisha usimamizi ili kulinda maisha ya watu na mali zao,” amesema Nkamba.

Zoezi la uokoaji linaendelea huku mamlaka husika zikichukua tahadhari zote muhimu ili kuhakikisha usalama katika eneo hilo unaendelea kudumishwa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!