Shauri la Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Geita, Neema Chozaire, lililokuwa linatarajiwa kusikilizwa kwa mara ya kwanza leo Julai 14, 2026, limeahirishwa baada ya Jeshi la Polisi kushindwa kumfikisha Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Geita.
Imeelezwa mahakamani kuwa sababu ya kutofikishwa kwa Chozaire ni kutokuwepo kwa mawakili wa Serikali ambao wapo Arusha kwa ajili ya mkutano wao. Kutokana na hali hiyo, Mahakama imeahirisha shauri hilo hadi Jumatatu, Julai 20, 2026.
Akizungumza nje ya mahakama, Wakili wa utetezi, Beatus Emmanuel, alisema Jaji Projestus Kahyoza, anayesikiliza shauri hilo, ameagiza Neema Chozaire afikishwe mahakamani bila kukosa saa 6:00 mchana, Julai 20, 2026.
“Kwa kuwa mleta maombi hakufikishwa mahakamani leo, mahakama imetoa amri kwamba afikishwe Julai 20, 2026 saa 6:00 mchana bila kukosa,” alisema Wakili Emmanuel.
Chozaire pia alitarajiwa kufikishwa mahakamani Julai 13, 2026, lakini hatua hiyo haikufanikiwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni sababu za kiutendaji. Leo tena, shauri hilo limeshindwa kuendelea kwa sababu ya kutokuwepo kwa mawakili wa Serikali.

Kwa upande wake, Katibu wa Chadema Kanda ya Ziwa Victoria, Zacharia Obadi, alisema chama hicho kimeendelea kushangazwa na sababu zinazotolewa mara kwa mara ambazo zimekuwa zikisababisha kiongozi huyo kutofikishwa mahakamani, licha ya kuwepo kwa amri halali ya mahakama inayotaka afikishwe.
Obadi alisema pia viongozi wa chama pamoja na ndugu wa Chozaire wamekuwa wakikosa fursa ya kumuona tangu aliposhikiliwa, jambo ambalo, kwa mujibu wake, linaongeza wasiwasi kuhusu mwenendo wa shauri hilo.
“Sasa tunasubiri Julai 20 kuona kama safari hii atafikishwa mahakamani kama ilivyoamriwa,” alisema Obadi.
Shauri hilo namba 15077 la mwaka 2026 lilifunguliwa Julai 8, 2026 na Chadema kupitia Wakili Beatus Emmanuel kwa hati ya dharura katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Geita.
Katika maombi yao, Chadema inaitaka Mahakama iamuru Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kufika mahakamani na kueleza sababu za Neema Chozaire kuendelea kushikiliwa bila kufikishwa mahakamani au kupewa dhamana.
Wengine waliotajwa katika shauri hilo ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita (RPC) na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO), ambao pia wanahusika kama wajibu maombi.