Na Theophilida Felician, Tanga.
Waganga wa tiba asili mkoani Tanga wameshauriwa kufuata misingi na mienendo mizuri aliyokuwa nayo aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Tiba Asili Tanzania (TAMESOT) Mkoa wa Tanga, marehemu Fadhili Ramadhani Mkomwa, aliyefariki dunia hivi karibuni, ili kuitumikia vyema taaluma hiyo.

Wito huo umetolewa na Katibu wa TAMESOT Mkoa wa Tanga, Rajabu Mlisi, wakati akisoma hotuba ya Katibu Mkuu wa chama hicho Taifa, Bw. Lukas Joseph Mlipu, katika tukio la kuhitimisha siku 40 za msiba wa mwenyekiti huyo lililofanyika nyumbani kwake, Kitongoji cha Kwichenje, Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa hotuba hiyo, marehemu Fadhili alitumikia tiba asili kwa kuzingatia misingi ya umoja, ushirikiano, uzalendo, upendo, na mshikamano- mambo yaliyomwongoza vyema na kumfanya kuwa kiongozi bora kwa wenzake kupitia TAMESOT.

Enzi za uhai wake, marehemu alitoa huduma ya tiba asili kwa jamii akizingatia sheria, kanuni, na taratibu zote zinazoelekezwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, jambo lililomfanya amalize mwendo wake salama duniani bila kukumbwa na misukosuko au kujihusisha na matendo maovu ndani ya taaluma hiyo.
Hali kadhalika, marehemu alikuwa akipenda kujielimisha kupitia mafunzo shirikishi yaliyoandaliwa na TAMESOT kwa kushirikiana na mamlaka za Serikali. Miongoni mwa mafunzo hayo ni pamoja na mafunzo kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kuhusu taratibu salama za uchakataji wa dawa asili. Pia alikuwa mshiriki mzuri wa Wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika inayofanyika mwezi Agosti kila mwaka, huku akionyesha kiu na dhamira ya kweli ya kuiendeleza tiba asili kwa vitendo.
Kupitia wasifu wa marehemu, hotuba hiyo imetoa wito kwa waganga wote nchini, wakiwemo wa Mkoa wa Tanga, kuendelea kutoa huduma inayokidhi viwango na kujitokeza kupata mafunzo maalum ili kujenga uwezo wao na kuepuka ukiukaji wa maadili.

Waganga na wananchi waliohudhuria wameungana kuendelea kutoa pole kwa familia, ndugu, na marafiki, huku wakimwombea marehemu Fadhili Ramadhani Mkomwa pumziko jema.