Latest Posts

PROF. SHIVJI AONESHA WASIWASI MASHITAKA KWA WAHADHIRI, SERIKALI YASISITIZA HAKUNA ALIYE JUU YA SHERIA

Katika andiko lake lililochapishwa kwenye wavuti ya taasisi ya kiuchunguzi ya CODESRIA, mwanasheria nguli na msomi mashuhuri wa sheria nchini Tanzania, Prof. Issa Shivji ameonesha wasiwasi mkubwa juu ya kile alichokiita msururu wa ukandamizaji na ukiukaji wa uhuru wa kifikra, akitolea mfano kukamatwa na kushitakiwa kwa mhadhiri msaidizi wa Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Melkisedeki Kitunzi Kaijage.

Prof. Shivji anafafanua kuwa Kaijage aliripoti kituo cha polisi Julai 8, 2026, akiambatana na mwanasheria wa Chama cha Wanataaluma UDOM (UDOMASA), kufuatia tuhuma za kuchochea maandamano ya siku ya mapumziko ya Saba Saba (Julai 7). Hata hivyo, baada ya kukaa mahabusu kwa siku 17 kinyume cha sharia na kufuatia amri ya Mahakama Kuu ya Julai 21 iliyoagiza apewe dhamana, Polisi tarehe 23 Julai walimfikisha Mhadhiri huyo Mahakama ya Hakimu Mkazi akituhumiwa kwa kosa la Ugaidi, kosa ambalo halina dhamana.

Hati ya mashtaka inamdai Kaijage kutishia kuchoma moto majengo ya umma na nyumba za polisi Julai 3, 2026. Prof. Shivji amekosoa hati hiyo akisema imekosa maelezo ya msingi kama vile eneo halisi vitisho vilipotolewa, chombo kilichotumika, na hadhira iliyokuwepo jambo linaloonesha matumizi ya mfumo wa mashtaka wa “kuchukua na kubandika” (cut-and-paste template) wenye lengo la kutisha wanataaluma na kupunguza uwezo wa vyuo vikuu kuwa vituo vya fikra tunduizi.

“Maelezo ya kosa katika hati ya mashtaka yanasomeka hivi: Melkisedek Kitunzi Kaijage, mnamo tarehe 03 mwezi Julai 2026 katika eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma ndani ya Mkoa wa Dodoma, alitenda kitendo cha kigaidi, yaani; kutishia kuchoma moto majengo ya umma na makazi ya askari polisi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa na nia ya kuwatisha kwa kiasi kikubwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mashtaka hayo yana tarehe ya Julai 22 yaani, siku moja baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu. Maelezo ya kosa hilo yanasomeka kana kwamba yamenukuliwa na kubandikwa tu (cut and pasted) kutoka kwenye muundo uleule wa siku zote. Yanakosa kabisa maelezo ya msingi na ya lazima yanayoweza kumwezesha mshtakiwa kujitetea dhidi ya tuhuma hizo. Ni wapi hasa chuoni hapo vitisho hivyo vilitolewa? Kwenye chumba cha mihadhara? Chini ya mti? Kwenye ukumbi wa umma? Je, vitisho hivyo vilikuwa vya maneno au vya maandishi? Ni njia gani iliyotumika kutoa tishio hilo, mitandao ya kijamii? Mhadhara? Mkutano wa hadhara? Wasikilizaji walikuwa kina nani, wanafunzi? Mpitanjia? Wafanyabiashara wa mtaani? Maneno halisi ya tishio hilo yalikuwa yapi? Maswali mengine mengi yanaweza kuulizwa lakini hayatakuwa na lazima. Lengo la mwandishi wa mashtaka hayo liko wazi- kwa makusudi ni kumshitaki Kaijage kwa kosa lisilokuwa na dhamana, si tu kwa ajili ya ‘kumwadhibu’ mshtakiwa, bali pia kupandikiza hofu na kuwatisha wanataaluma wenzake”, ameandika Prof. Shivji na kuongeza,

“Hakuna Mtanzania mwenye timamu za akili anayeweza kufikiria kuwa mhadhiri wa chuo kikuu anaweza kutoa tishio la kuchoma moto majengo ya umma na makazi ya polisi. Lakini ndio hapo tulipo! Tunaambiwa kuwa hata baada ya machafuko ya uchaguzi mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025 yaliyosababisha viumbe na vifo vya mamia ya vijana, na hofu kuu iliyotanda kote nchini baada ya hapo, bado kuna Mtanzania mmoja aliyejitenga mwenye ujasiri wa kutoa vitisho vya kuchoma majengo ya umma na makazi ya polisi”.

Prof. Shivji ameongeza kuwa visa kama hivyo vimewakumba pia wahadhiri wa Chuo Kikuu cha St. John’s cha Dodoma (Johaiven Bikongolo na Titus Kituli), pamoja na viongozi na wanachama wa chama cha upinzani cha CHADEMA, wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu. Shivji amehoji pia ukimya wa UDASA (Chama cha Wanataaluma UDSM) huku akitoa wito kwa wanataaluma Barani Afrika kutokubali kunyamazishwa.

Akitolea ufafanuzi malalamiko na namna hiyo na taarifa za kukamatwa kwa watuhumiwa zaidi ya 130 kote nchini, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, akizungumza tarehe 29 Julai 2026 visiwani Zanzibar, amekanusha vikali kuwa kuna mkakati wa kiserikali wa kulenga kundi fulani, wanataaluma, au taasisi ya kisiasa.

Waziri Katambi alisisitiza kuwa Jeshi la Polisi lilichukua hatua za kuzuia viashiria vya uvunjifu wa amani vilivyopangwa na kuratibiwa kuelekea siku ya Saba Saba, baada ya kutoa tahadhari zaidi ya nne kwa umma.

“Lakini pia kama walitaka kulenga labda wanataaluma wangeweza kukamata…kuna wanataaluma ambao wako huru mpaka sasa, kwahiyo tusitetee vitu ambavyo hatuvijui na hasa kwenye mashauri ambayo yako mahakamani, kwa sasa hatuna nguvu ya kuyahoji kwa sababu…nimesikia kuna mahali wanasema kuna Uganda Convention ambayo siyo kinga ya jina yaani unapokuwa mhadhiri, unapokuwa mwanasheria, unapokuwa waziri, unapokuwa mbunge, unapokuwa mfanyabiashara au mwanasiasa, unapokuwa mkulima, mfugaji, mtu awe yeyote hakuna mtu aliye juu ya sheria”, alisema Katambi.

Alimalizia kwa kuwataka wananchi na mitandao ya kijamii kuacha kupotosha umma na badala yake kuziachia mahakama zifanye kazi yake kwa mujibu wa misingi ya kisheria na Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayomtambua mtu kuwa hana hatia hadi mahakama itakapothibitisha vinginevyo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!