Latest Posts

TISEZA NA VODACOM ZAINGIA MKATABA WA KIDIJITI; KUKUZA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI NCHINI

Katika jitihada za kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kuvutia mitaji zaidi nchini, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) na kampuni ya Vodacom Tanzania PLC, leo Agosti 11, 2026, zimesaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) wa miaka miwili kwa ajili ya kuunganisha huduma za uwekezaji na masuluhisho ya kisasa ya kiteknolojia.

Ushirikiano huo unalenga kutoa huduma bora kwa wawekezaji kupitia miundombinu ya kidijitali kama vile teknolojia ya mtandao wa vifaa (Internet of Things – IoT), internet isiyohamishika, na mifumo ya malipo ya kielektroniki ili kurahisisha uwekezaji.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri, ameeleza kuwa ushirikiano huo unalenga kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye muitikio rafiki kwa wawekezaji kwa kutumia utaalamu wa Vodacom katika sekta ya mawasiliano.

“Lengo la ushirikiano wetu ni kuendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini lakini pia kuunganisha dhamana ambayo sisi tunayo ya kukuza, kuratibu na kuwezesha uwekezaji pamoja na utaalam ambao wenzetu wanao kwenye masuala ya teknolojia na masuluhisho ya kidijiti,” amesema Teri

Ameongeza kuwa ushirikiano huu ni utekelezaji wa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa tarehe 3 Agosti, 2026, akisisitiza kuwa sekta binafsi ndiyo ufunguo wa kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, amewahakikishia wawekezaji kuwa kupitia ushirikiano huu, wataweza kupata huduma zilezile za kiteknolojia zinazopatikana katika mataifa yaliyoendelea kwasababu Vodacom ni sehemu ya familia ya kimataifa ya Vodafone.

“Wawekezaji wanatakiwa wajue chochote walichoweza kukifanya wakiwa Ureno basi kinaweza kufanyika Tanzania. Chochote alichoweza kukifanya kwenye kiwanda chake kilichopo Ujerumani basi kinaweza kufanyika Tanzania kwa sababu sisi ni familia moja,” amesisitiza Kamando.

Aidha, Kamando amebainisha kuwa Vodacom itatoa huduma za ulinzi dhidi ya udukuzi wa mitandaoni na mifumo ya malipo isiyotumia fedha taslimu kwa wawekezaji wakubwa na wadogo ili kuongeza ufanisi na usalama wa miamala.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!