Wafugaji wa Kata ya Shiloleli, Manispaa ya Geita, wamemshukuru Mbunge wa Geita Mjini, Mhandisi Chacha Wambura, kwa kutekeleza ahadi yake ya kutoa Sh milioni 1.5 kwa ajili ya upatikanaji wa dawa za kuogeshea mifugo.
Wafugaji hao wamesema msaada huo umewawezesha kupata dawa zinazotumika katika kuogesha mifugo mbalimbali, ikiwemo ng’ombe, mbuzi na kondoo, hatua ambayo itasaidia kudhibiti wadudu na magonjwa yanayoweza kuathiri afya ya mifugo.

Hatua hiyo imekuja baada ya Afisa Mifugo wa Kata ya Shiloleli, kwa niaba ya wananchi, kumuomba Mbunge Wambura kusaidia upatikanaji wa dawa za kuogeshea mifugo katika josho lililopo katika eneo hilo.
Akijibu ombi hilo, Mhandisi Chacha Wambura aliahidi kuhakikisha kuwa ndani ya kipindi cha miezi sita anagharamia upatikanaji wa dawa hizo, ili kuwawezesha wafugaji kuendelea na huduma ya uogeshaji wa mifugo bila kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa dawa.

Ahadi hiyo sasa imetekelezwa baada ya Mbunge huyo kutoa Sh milioni 1.5 kwa ajili ya ununuzi wa dawa hizo, ambazo tayari zimeanza kutumika katika zoezi la kuogesha mifugo katika Kata ya Shiloleli.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa zoezi hilo, Daktari wa Mifugo wa Manispaa ya Geita Jeremia Njile amesema uogeshaji wa mifugo ni muhimu katika kudhibiti wadudu wanaosababisha magonjwa mbalimbali kwa mifugo.

Amesema hatua iliyochukuliwa na Mbunge Wambura ya kuhakikisha dawa zinapatikana itakuwa na manufaa makubwa kwa wafugaji, kwa kuwa itawawezesha kutekeleza zoezi la uogeshaji kwa wakati na hivyo kulinda afya ya mifugo yao.
Kwa upande wao, wafugaji hao wamepongeza hatua hiyo, wakisema upatikanaji wa dawa utawasaidia kuimarisha shughuli zao za ufugaji na kupunguza changamoto zinazotokana na magonjwa ya mifugo.
Kata ya Shiloleli inajumla ya Ng’ombe 3647,Mbuzi 1420 na Kondoo ni zaidi ya mia Tisa.
