Waangalizi wa kimataifa wa Uchaguzi Mkuu nchini Zambia, wakiwamo kutoka Umoja wa Ulaya (EU) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), wameonesha wasiwasi mkubwa kufuatia taarifa za matukio ya vurugu, utekaji, na kusimamishwa kwa muda kwa zoezi la kuhesabu kura.
Hatua hiyo inakuja baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zambia (ECZ) kusitisha kwa saa kadhaa zoezi la kuhesabu kura siku ya Ijumaa kufuatia mashambulizi dhidi ya makatibu wa vituo na madai ya kuibiwa kwa karatasi za kura, kabla ya kurejesha tena zoezi hilo baada ya kueleza kuwa ulinzi umeimarishwa.
Kinyang’anyiro hicho kinamkutanisha Rais aliyepo madarakani, Hakainde Hichilema (64) wa chama tawala cha United Party for National Development (UPND), anayewania muhula wa pili, dhidi ya mpinzani wake mkuu, Brian Mundubile (55), aliyekuwa waziri wa zamani kupitia chama cha Patriotic Front (PF) na sasa anagombea kupitia muungano wa National Reconciliation Party for Unity and Prosperity (NRPUP).
Mundubile amekosoa vikali uamuzi wa kusimamisha kuhesabu kura akisema unaleta shaka ya kuwepo kwa “mchezo mchafu wa kubadili matokeo.” Hata hivyo, Mkurugenzi wa Habari wa Kampeni za Hichilema, Mark Simuuwe, ameyakataa madai hayo na kusema upinzani unateswa na hofu kwasababu matokeo ni halali.
Kiongozi wa Timu ya Waangalizi wa SADC, Samuel Tembenu (aliyekuwa Waziri wa Sheria wa Malawi), ameeleza kuwa timu yake haikuweza kushuhudia uhesabuji wa kura wakati wa sitisho hilo, huku akibainisha kupokea ripoti za kujeruhiwa kwa watu, uharibifu wa mali, utekaji, na kifo cha msimamizi mmoja wa kura:
“Kusitishwa kwa zoezi hilo kumeleta taharuki na wasiwasi mkubwa. Tumepokea taarifa za vitendo vya vitisho, utekaji na angalau kifo cha mtu mmoja katika mikoa mitano, ingawa bado tunajiridhisha kwa kina. Tunasihi pande zote zitulie,” aMEsema Tembenu.
Naye Mkuu wa Waangalizi wa Umoja wa Ulaya (EU), Michael McNamara, na Mkuu wa Ujumbe wa Bunge la Ulaya, Reinhold Lopatka, wametoa wito kwa serikali kutoa maelezo ya kina kuhusu uamuzi huo wa kusimamisha kura ambao wameutaja kama “usio na uwiano” kwa kuwa ni vituo vichache tu kati ya zaidi ya 13,000 vilivyoathirika na vurugu.
Jeshi la Polisi nchini Zambia limethibitisha kuwakamata watu 9 wakituhumiwa kuhusika na mauaji ya msimamizi wa kura mwenye umri wa miaka 57 katika mji mmoja karibu na Lusaka.
Hadi kufikia mwishoni mwa Jumamosi, Tume ya Uchaguzi (ECZ) ilikuwa imetangaza matokeo ya awali kutoka majimbo 49 kati ya 226, ambapo matokeo hayo yasiyo ya mwisho yanaonesha kuwa Hakainde Hichilema (UPND) alikuwa na kura 438,708 (Sawa na 52.6%), Brian Mundubile (NRPUP): Kura 351,281 (Sawa na 42.1%), na Kelvin Bwalya (ZMBP): Kura 3,965.
Mundubile tayari ametangaza ushindi akitaja matokeo ya kituo chake cha majumuisho na kudai jeshi limeingilia vituo vya majumuisho vya Mufulira. Hichilema hajaandika ushindi lakini amesema takwimu za mwanzo “zinatoa matumaini makubwa.”
Hali ya usalama imezidi kuimarishwa katika mji mkuu wa Lusaka, ambapo askari wa jeshi na polisi wakiwa na magari ya kivita wametanda mtaani, huku Tume ya Uchaguzi ikitarajiwa kutoa taarifa zaidi kuhusu muda rasmi wa kutangaza matokeo ya mwisho.