Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amewataka vijana kutumia michezo kama fursa ya kujipatia ajira na kujenga maisha yao, huku wakiepuka vitendo vya uhalifu ikiwemo wizi na ukatili wa kijinsia.
Mahundi ameyasema hayo wakati akikabidhi vifaa vya michezo kwa timu 13 za Kata ya Iwambi jijini Mbeya, huku akisisitiza kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kuwaweka vijana pamoja, kukuza vipaji, kuimarisha amani na mshikamano katika jamii.
Aidha, amependekeza kuanzishwa kwa klabu ya mbio za polepole (jogging) katika kata hiyo, akisema mazoezi ni muhimu katika kuimarisha afya na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
Amesema michezo inapaswa kuwa chombo cha kuimarisha upendo na mshikamano ndani na nje ya Kata ya Iwambi, huku akiwataka wananchi kushirikiana katika mapambano dhidi ya uhalifu.

Mahundi, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya na Mkurugenzi wa Maryprisca Women Empowerment Foundation (MWEF), amekabidhi jozi mbili za vifaa vya michezo kwa kila timu pamoja na mpira mmoja kwa kila timu.
