Latest Posts

WALIOPATA, WALIOKOSA USHINDANI WA SOKO LA MAFUTA NCHINI

Ushindani katika soko la mafuta nchini Tanzania umeongezeka katika mwaka wa fedha wa 2024/25, huku kampuni ya Camel Oil ikiibuka kama iliyopiga hatua kubwa zaidi wakati baadhi ya wachezaji wa zamani wakipoteza sehemu kubwa ya soko, kulingana na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).

Kwa mujibu wa habari ya mwandishi Gadiosa Lamtey iliyochapishwa na The Citizen, ripoti ya Utendaji wa Sekta Ndogo ya Mafuta ya Ewura kwa mwaka 2024/25 inaonesha kuwa makampuni matano makubwa ya usambazaji wa mafuta (OMCs) yalidhibiti asilimia 48.7 ya soko la mafuta, ikiiachia asilimia 51.3 kwa wachezaji wengine.

Puma Energy iliendelea kuwa kinara wa soko ikiwa na hisa ya asilimia 15.5, ikifuatiwa na Camel Oil yenye asilimia 11.4, Mansoor Industries Limited (MOIL) ikiwa na asilimia 10, Oilcom Tanzania yenye asilimia 6.4, na Mount Meru Petroleum ikiwa na asilimia 5.3.

Takwimu hizo zinaonesha mabadiliko makubwa miongoni mwa wachezaji wakuu, hasa Camel Oil, ambayo ilipanda kutoka nafasi ya walio shika nafasi ya nane mwaka 2023/24 hadi nafasi ya pili mwaka 2024/25. Hisa yake ya soko iliongezeka zaidi ya mara mbili kutoka asilimia 5.54 hadi asilimia 11.4.

“Puma Energy imeweka msimamo wa kushikilia nafasi ya kwanza kwa kipindi cha miaka ane, wakati Camel Oil imetoka nafasi ya nane ikiwa na hisa ya soko ya asilimia 5.54 katika Mwaka wa Fedha 2023/24 hadi nafasi ya pili ikiwa na hisa ya asilimia 11.4,” inasema ripoti hiyo.

Mabadiliko hayo hayakugusa Camel Oil pekee. MOIL, ambayo iliyokuwa ya pili kwa ukubwa, ilishuka hadi nafasi ya tatu baada ya hisa yake ya soko kupungua kutoka asilimia 11.12 mwaka 2023/24 hadi asilimia 10 mwaka 2024/25.

Acer Petroleum nayo ilikutana na mporomoko mkubwa, ambapo hisa yake ilishuka kutoka asilimia 7.96 hadi asilimia 4.8, hatua iliyoisukuma kutoka nafasi ya nne hadi ya nane. Oryx Oil ilirekodi anguko jingine kubwa, hisa yake ikishuka kutoka asilimia 5.99 hadi asilimia 2.8, na kuporomoka kutoka nafasi ya sita hadi ya 11. Mount Meru Petroleum, kwa upande wake, iliongeza hisa yake hadi asilimia 5.3 na kujitwalia nafasi ya tano.

 

Kipi Kinachotawala Ukuaji wa Hisa ya Soko?

Ewura ilisema hisa ya soko inaathiriwa na mambo kadhaa badala ya idadi tu ya makampuni yanayofanya kazi katika sekta hiyo. Mambo haya ni pamoja na idadi ya vituo vya mafuta vinavyomilikiwa na kampuni (retail outlets), uaminifu wa wateja kwa chapa fulani (brand loyalty), ubora wa huduma zinazotolewa kwa vituo vya mafuta vinavyojitegemea na mikataba ya usambazaji na wateja wakubwa (viwanda, shughuli za uchimbaji madini, na biashara za kilimo).

Mkurugenzi wa Sekta ya Mafuta wa Ewura, Gerald Maganga, ameeleza kuwa takwimu hizi zinaonesha sekta hiyo ina ushindani wa kweli na uwepo wa wachezaji wengi unalinda soko dhidi ya uhaba wa mafuta pindi kampuni moja inapojitoa.

Hata hivyo, Ewura imesisitiza kuwa makampuni yanazuiwa kujihusisha na vitendo vinavyovunja ushindani wa haki, ikiwa ni pamoja na kuchafua au kushusha viwango vya ubora wa mafuta, kuuza bidhaa za mafuta juu ya bei kikomo zilizoainishwa na serikali, kukiuka masharti ya afya, usalama, na mazingira (HSE).

Naye, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Deogratius Massawe, amesema ukuaji wa makampuni ya ndani ni hatua chanya inayoongeza ustahimilivu wa kiuchumi. Ameonya kuwa kutegemea zaidi makampuni ya kigeni kunaweza kuingiza nchi kwenye mshtuko wa kiuchumi pale makampuni hayo yanapokabiliwa na vikwazo vya kimataifa.

Kupaa kwa Camel Oil kutoka nafasi ya 8 hadi ya 2, na kuendelea kushikilia nafasi za juu kwa makampuni kama MOIL na Oilcom, ni ishara ya wazi kuwa makampuni ya ndani ya Kitanzania yameongeza uwezo wa kimitaji, usimamizi, na mtandao wa kibiashara. Mwelekeo huu unajibu moja kwa moja mijadala yetu iliyopita kuhusu Local Content na sheria za uwezeshaji wazawa-w azawa sasa hawapo tena kwenye karatasi tu, bali wanamiliki sekta za kimkakati.

Kwa upande mwingine, kuporomoka kwa hisa za soko za makampuni makubwa ya kimataifa kama Oryx Oil (kutoka nafasi ya 6 hadi ya 11) na mabadiliko ya kibiashara ya Puma Energy kunadhihirisha mabadiliko ya mtazamo wa uwekezaji duniani. Kama alivyobainisha kiongozi wa TPSF, vikwazo vya kijiografia na kisiasa pamoja na mabadiliko ya usimamizi wa kisheria vinayafanya makampuni ya ndani kuwa salama zaidi kulinda usalama wa nishati nchini.

Sekta ya mafuta na nishati ndiyo mhimili mkuu wa usafirishaji, uzalishaji viwandani, na sekta ya kilimo. Mabadiliko haya chanya katika sekta binafsi yanaimarisha safari ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambapo serikali inalenga kuifanya sekta binafsi (hususan ya wazawa) kuchangia asilimia 70 ya uchumi. Ushindani huu huru unaosimamiwa na Ewura unalinda walaji dhidi ya ukiritimba na kuhakikisha mafuta yanapatikana kwa bei na viwango vinavyokubalika nchi nzima.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!