Latest Posts

TANZANIA NA UMOJA WA ULAYA ZAZINDUA MIKAKATI YA KUVUTIA MITAJI: MKAZO KUWEKWA KWENYE ONGEZEKO LA THAMANI NA MADINI YA KIMKAKATI

Serikali ya Tanzania, kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU), imezindua rasmi maandalizi ya ziara maalum ya kibiashara na uwekezaji (European Roadshows) itakayofanyika katika nchi nne za Ulaya, ikiwa na lengo la kuvutia mitaji mikubwa na kuimarisha ongezeko la thamani kwa bidhaa za Tanzania

Ziara hiyo, ambayo ni sehemu ya awamu ya kwanza ya Jukwaa la Uwekezaji na Biashara kati ya Umoja wa Ulaya na Tanzania (2026-2027), itafanyika kuanzia tarehe 28 Septemba hadi 6 Oktoba 2026 katika nchi za Finland, Italia, Uholanzi, na Ubelgiji. Maeneo yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na kilimo, madini ya kimkakati, uchumi wa kidijiti, nishati mbadala, na miundombinu ya usafirishaji.

Akizungumzia umuhimu wa ziara hiyo wakati wa Jukwaa la Uwekezaji na Biashara kati ya Umoja wa Ulaya na Tanzania Agosti 18, 2026, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wawekezaji kutoka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), James Maziku, ameeleza kuwa lengo ni kuunganisha sekta binafsi ya Tanzania na ya Ulaya.

“Tunataka kufika mahala tuunganishe mitaji ya sekta binafsi kutoka bara la Ulaya kuja kuwekeza kwenye sekta ya kilimo ili kuweza kufungamanisha kilimo na ongezeko la thamani,” amesema Maziku

Ameongeza kuwa katika sekta ya madini, Tanzania inalenga kuvutia mitaji kwa ajili ya madini ya kisasa kama kinywa, lithium, na cobalt ili kupunguza uuzaji wa madini ghafi.

Naye Balozi John Ulanga kutoka Idara ya Diplomasia ya Uchumi (Wizara ya Mambo ya Nje), amebainisha kuwa ziara hiyo ni ishara ya imani ya kimataifa kwa uchumi wa Tanzania, akieeleza pia kuwa nchi kama Italia zina hamu kubwa ya kuwekeza katika kilimo cha mpunga, kahawa, na korosho, kwa msisitizo wa ufungashaji na usindikaji nchini.

“Hii ni dalili ya ushirikiano mzuri na dalili ya imani ambayo wamekuwa nayo kwenye mazingira ya uwekezaji na mazingira ya uchumi kwa ujumla kwa nchi yetu,” amesema Balozi Ulanga

Kwa upande wake, Mkuu wa Ushirikiano wa Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na EAC, Marc Stalmans, amesisitiza kuwa ushirikiano huu mpya unalenga kuleta manufaa ya pande zote kwa kuhakikisha kuwa usindikaji wa bidhaa unafanyika hapa nchini badala ya kuuza malighafi nje.

“Manufaa ya mabadiliko hayo yanapaswa kubaki katika mifuko ya Watanzania… Soko la Ulaya litapata bei nzuri na ubora ule ule huku likijua bidhaa inatoka Tanzania, na mkulima mdogo pamoja na serikali ya Tanzania watanufaika,” amesema Stalmans

Ziara hizi zitahusisha mikutano ya ana kwa ana kati ya wafanyabiashara (B2B) na kati ya serikali na wafanyabiashara (B2G), na zinatarajiwa kuhitimishwa na Jukwaa kubwa la Uwekezaji jijini Dar es Salaam mapema mwaka 2027.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!