Zahanati ya Mwatulole iliyopo Kata ya Buhalabahala, Wilayani Geita, inakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa huduma ya umeme na maji kwa muda mrefu, hali inayotajwa kuathiri utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo. Zahanati hiyo pia haina uzio unaoweza kusaidia kuimarisha usalama wa eneo la kituo na kudhibiti vitendo vya wizi.
Kutokana na hali hiyo, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Mhandisi Chacha Wambura, ametembelea zahanati hiyo kwa lengo la kujionea hali ya utoaji wa huduma na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, wananchi pamoja na Mwenyekiti wa Mtaa wameeleza kuwa ukosefu wa umeme na maji ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazokikabili kituo hicho, huku wakiiomba Serikali na wadau wengine kusaidia kutatua changamoto hizo.
Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Mhandisi Chacha Wambura, amesema dhamira yake ni kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi zinapatiwa ufumbuzi, akiahidi kushughulikia upatikanaji wa umeme katika zahanati hiyo pamoja na kuwezesha upatikanaji wa maji.

Amesema huduma hizo ni muhimu katika kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za afya na kuhakikisha wananchi pamoja na watumishi wa zahanati hiyo wanapata mazingira bora ya kuhudumia na kupata huduma.
Wananchi wameeleza matumaini kuwa utekelezaji wa ahadi hiyo utasaidia kuboresha huduma za afya katika Zahanati ya Mwatulole na kupunguza changamoto zinazowakabili kwa muda mrefu.
