Kesi ya uhaini namba 19605/2025 inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Antiphas Lissu, imeshika kasi kubwa mchana wa Agosti 26, 2026, baada ya kurejea kwa ajili ya maswali ya dodoso (cross-examination) ambapo Lissu kama shahidi wa kwanza amedodoswa na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassor Katuga, ambapo mwanasiasa huyo amekiri kuwa kauli za ‘tutakinukisha’ ni zake lakini akasisitiza kuwa hazina shida yoyote kisheria wala hazitengenezi kosa la uhaini.
Joto la maswali hayo ya dodoso lilianza pale Wakili wa Serikali Mkuu alipotaka Lissu athibitishe kama anatambua kuwa Tanzania ni nchi huru iliyopata uhuru Desemba 9, 1961, na kama Mahakama ndicho chombo cha mwisho cha maamuzi ya kisheria. Lissu amekiri kuwa Mahakama hailazimishwi na mamlaka yoyote ya ndani au nje inapotoa uamuzi yake.
Alipoulizwa kama wadhifa wake kama Mwenyekiti wa CHADEMA unampa kinga ya kutoshtakiwa, Lissu alijibu: “Sijaiambia mahakama hiyo, na sina hakika na hilo.
Upande wa serikali ulihoji sababu za Lissu kutoleta tuzo zake za kimataifa (kama vile Bush-Thatcher Award ya IDU) mahakamani kama thibitisho la sifa alizojigambia nazo kizimbani. Lissu alijibu kuwa hana wajibu huo kisheria, “Mimi sina wajibu wa kuthibitisha chochote”.
Katika hatua nyingine, Wakili wa Serikali alimuuliza Lissu kama anakataa maneno yaliyo kwenye hati ya mashtaka yanayosema ” Wanasema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli”. Lissu alijibu kuwa ili kuelewa maneno hayo, ni lazima mtu aelewe hotuba nzima. Wakili aliendelea kumuuliza kama maneno hayo ni yake au la, Lissu alijibu “Maneno ni ya kwangu, na hayana shida”.
Wakili wa Serikali alimuuliza Lissu kama ana chuki binafsi dhidi ya serikali kutokana na mfululizo wa mapambano yake ya kisiasa. Lissu hakumung’unya maneno bali alijibu thabiti, “Nina chuki dhidi ya uonevu, nina chuki na serikali inayoonea watu”.
Aidha, Wakili wa serikali aliunganisha kauli ya Lissu na fujo za uchaguzi zilizodaiwa kupangwa na baadhi ya watu, akirejea ushahidi wa PW13 aliyesema walipanga kuzuia uchaguzi kwa kuwapiga mawe wapiga kura. Lissu alijibu kuwa kupiga mawe wapiga kura ni uvunjifu wa amani na uvunjaji sheria. Hata hivyo, alisisitiza kuwa yeye alihamasisha maandamano ya kidemokrasia yaliyolindwa kikatiba chini ya Ibara ya 20. Alitetea msimamo wa kuzuia uchaguzi usio wa haki akieleza kuwa kuzuia uchaguzi mbovu kwa njia za kikatiba kunaruhusiwa kwa sababu Katiba haina Ibara moja tu, na hii ni baada ya mawakili wa serikali kumwambia Lissu kama anafahamu kuzuia uchaguzi ni kwenda kinyume cha katiba
Mvutano huo ulifikia ukomo saa 11:00 jioni kutokana na muda wa mahakama kuisha. Jopo la majaji limeahirisha shauri hilo hadi kesho yake, Agosti 27, 2026, saa tatu kamili asubuhi, ambapo maswali hayo ya dodoso yataendelea.