Jamii imetakiwa kushirikiana kwa pamoja kukemea mmomonyoko wa maadili ili kujenga jamii salama yenye kuzingatia mila, desturi na tamaduni za Kitanzania.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 29, 2026, mkoani Morogoro na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, wakati akifunga Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni.
Msigwa amesema ni wakati sasa wa jamii kuwatumia machifu na viongozi wa kimila katika kulinda na kuenzi maadili, mila na desturi za Kitanzania, akisisitiza kuwa utamaduni ni sehemu muhimu ya utambulisho na utaifa wa Tanzania.

Aidha, Msigwa ametoa wito kwa wananchi kutumia mitandao ya kijamii kwa manufaa ya jamii na taifa, badala ya kuitumia kama sehemu ya kukiuka maadili, akieleza kuwa mitandao hiyo inaweza kutumika kukuza fursa za kiuchumi na kutangaza utamaduni wa Tanzania.
Katika hatua nyingine, Msigwa amewataka wananchi kutumia fursa zinazotokana na michuano ya AFCON kwa kufanya biashara mbalimbali, ikiwemo biashara za bidhaa za kitamaduni na huduma, ili kunufaika kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Sebastian Waryuba, amesema Mkoa wa Morogoro umejivunia kuwa mwenyeji wa Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni, akieleza kuwa tamasha hilo limekuwa fursa ya kuonesha utajiri wa mila, desturi, sanaa na utamaduni kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Katika mashindano ya ngoma za asili yaliyofanyika katika tamasha hilo, Mkoa wa Mwanza umeibuka mshindi wa kwanza, ukifuatiwa na Mkoa wa Mtwara ulioshika nafasi ya pili, huku Mkoa wa Dodoma ukichukua nafasi ya tatu.

Kwa upande wa mashindano ya vyakula vya asili, Mkoa wa Iringa umeibuka mshindi wa kwanza, ukifuatiwa na Mkoa wa Pwani ulioshika nafasi ya pili, huku Mkoa wa Singida ukichukua nafasi ya tatu.
Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni limekuwa jukwaa muhimu la kuonesha utajiri wa tamaduni za Tanzania, kukuza umoja na utaifa, pamoja na kutoa fursa kwa wananchi kutumia utamaduni na ubunifu katika kujiletea maendeleo ya kiuchumi.
