Taasisi isiyo ya kiserikali ya Lebao’s Kids Foundation imejenga shule kwa ajili ya watoto yatima wanaolelewa katika Kituo cha Watoto Yatima cha Familia Takatifu, Marcellino Corradini, kilichopo Migoli mkoani Iringa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za elimu na ustawi wa watoto hao.
Mkurugenzi mwenza na mfadhili mkuu wa Taasisi hiyo, Catherine Moreno, amesema ujenzi wa shule hiyo umelenga kupunguza changamoto ambazo watoto hao walikuwa wakikabiliana nazo, ikiwemo kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya elimu, hali ambayo ilikuwa ikiweka usalama wao hatarini.

Amesema uwepo wa shule hiyo karibu na kituo utawasaidia watoto kupata elimu katika mazingira salama na rafiki, huku wakipunguza muda na changamoto walizokuwa wakikumbana nazo katika safari za kwenda na kurudi shuleni.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Lebao’s Kids Foundation, Theophil Muyinga, amesema taasisi hiyo imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kuwasaidia watoto hao wenye uhitaji na kurejesha furaha katika maisha yao.
Muyinga amesema mbali na ujenzi wa shule, taasisi hiyo imetekeleza miradi ya maji na umeme pamoja na ukarabati wa majengo ya kituo hicho, akieleza kuwa mradi wa elimu ni mwendelezo wa juhudi za taasisi hiyo katika kuboresha mazingira ya malezi na makuzi ya watoto hao.

Uongozi wa Kituo cha Watoto Yatima cha Marcellino Corradini ukiwakilishwa na Sr Marcelina Assenga ambaye ni Msimamizi wa kituo hicho umeipongeza Lebao’s Kids Foundation kwa msaada huo, ukieleza kuwa miradi iliyotekelezwa imekuwa na mchango mkubwa kwa watoto huku wakiutaja mradi wa maji kuwa miongoni mwa miradi iliyowasaidia watoto kuondokana na changamoto ya kuamka asubuhi na kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji.
Shule hiyo mpya itatoa kipaumbele kwa watoto wanaoishi katika kituo hicho, huku watoto wengine kutoka maeneo ya jirani wakikaribishwa kupata huduma ya elimu, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za elimu kwa jamii inayozunguka kituo hicho.
Watoto wanaolelewa katika kituo hicho wameishukuru Lebao’s Kids Foundation kwa kuwajengea shule hiyo na kuahidi kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao na kuwa na mchango chanya katika jamii.