DAR ES SALAAM: Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) na Tanzania Chefs Alliance wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika kukuza vipaji vya upishi, kupitia mashindano ya kitaifa na shughuli mbalimbali za kitaalamu katika sekta ya ukarimu.
Akizungumza kuhusu ushirikiano huo, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Dkt. Florian Mtey, amesema lengo si kuwa na makubaliano yanayobaki kwenye karatasi, bali kuhakikisha yanazaa matokeo yanayoweza kuonekana katika sekta ya upishi nchini.
“Tunaposaini makubaliano haya ni matarajio yetu sio kubaki na hati nzuri yenye saini, bali ni kuona matokeo yanayoonekana,” amesema Dkt. Mtey.

Amesema kupitia ushirikiano huo, wanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Utalii watapata fursa zaidi za kushiriki katika mashindano na shughuli za kitaalamu, huku wataalamu wa sekta hiyo wakipata nafasi ya kubadilishana uzoefu na maarifa.
Kwa mujibu wa Dkt. Mtey, ushirikiano huo pia unatarajiwa kusaidia kugundua na kulea vipaji vipya, kuongeza ubunifu katika upishi pamoja na kuipa nafasi kubwa zaidi chakula cha Tanzania kutangazwa ndani na nje ya nchi.
“Tunatarajia kuona wanafunzi wetu wakipata fursa zaidi za kushiriki katika mashindano na shughuli za kitaalamu. Wataalamu wetu wakibadilishana uzoefu, vipaji vipya vikigunduliwa na kulelewa, ubunifu katika upishi ukiongezeka, na chakula cha Tanzania kikitangazwa zaidi ndani na nje,” amesema.
