Latest Posts

KESI YA UHAINI YA LISSU: HECHE ABANWA NA BARUA ZA WITO WA TUME YA JAJI CHANDE MAHAKAMANI

Baada ya shahidi wa tano katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, kuiambia Mahakama kwamba hakuwahi kuitwa na Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 (Tume ya Jaji Chande), Wakili wa Serikali Mkuu Nassor Katuga amemuonesha nyaraka ambazo ni barua zilizomtaka kufika mbele ya tume hiyo.

Shahidi huyo ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, amesisitiza msimamo wake wa awali akidai kuwa hakuwahi kupokea wito wowote rasmi kutoka kwa chombo hicho cha uchunguzi ingawa Wakili wa Serikali Mkuu, Nassor Katuga aliomba ridhaa ya Mahakama na kumkabidhi mfululizo wa nyaraka ambazo zilikuwa ni barua ili kuupima ukweli wa kauli yake, ambapo Heche alizipokea, kuzitazama na kuzisoma mbele ya jopo la majaji.

Katika uchunguzi huo wa vielelezo, Heche alithibitisha kuwa barua ya kwanza ilitaja sanduku la posta 31191 linalomilikiwa na chama hicho. Wakili Katuga aliendelea kumuuliza shahidi huyo kwa kumwonesha barua ya pili na ya tatu, ambapo Heche alilazimika kusoma vichwa vya habari vilivyothibitisha wito wa wazi wa kutakiwa kukutana na tume hiyo ya Rais kuzungumzia matukio hayo ya Oktoba 2025.

Licha ya kubanwa na vielelezo hivyo vya kimaandishi ambavyo amesema pia vilielekezwa pia kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Heche alikataa katakata pale alipoulizwa kama angetaka barua hizo zipokelewe rasmi kama ushahidi wa kesi hiyo mahakamani hapo.

Katuga alimuuliza heche pia kama alikuwa na ufahamu kuwa Tume hiyo ilitoa tangazo kwa umma ikiruhusu kuwasilisha ushahidi kwa tume hiyo kuhusu matukio ya Oktoba 29, 2025 kupitia njia mbalimbali za kidijiti kama SMS, WhatsApp na barua pepe kwa wasiotaka kufika mbele ya Tume hiyo ambapo Heche akasema hakuwa na ufahamu huo.

Heche alihitimisha kwa kufafanua kuwa msimamo wao haukuwa kukataa kutoa ushirikiano kwa ujumla, bali walipinga wazi muundo uliotumika kuunda Tume hiyo ya Jaji Chande.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!