Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Qwaray, amewataka watumishi wa umma nchini kuongeza matumizi ya mifumo ya kidijiti ili kupunguza urasimu na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Qwaray ametoa agizo hilo leo Septemba 17, 2026 wakati akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri za Manispaa na Wilaya ya Geita mkoani Geita kwa lengo la kusikiliza changamoto za watumishi na kujadili namna ya kuboresha utendaji katika Utumishi wa Umma

Amesema matumizi sahihi ya teknolojia ya TEHAMA ni muhimu katika kuongeza kasi ya utendaji na uwajibikaji katika utumishi wa umma na itasaidia kuchagiza jitihada za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Wajibu wetu wa kwanza chini ya Dira hii mpya ni kuongeza kasi ya utendaji, kukumbatia kikamilifu mifumo ya kidijiti ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa umma kwa wakati na bila usumbufu,” amesema.
Aidha, amebainisha kuwa mfumo wa e-Watumishi na Watumishi Portal inawezesha watumishi kupata huduma mbalimbali za kiutumishi kwa njia ya mtandao ikiwa ni pamoja na taarifa za mishahara, likizo na uhamisho, hivyo, amewataka kuitumia kwa makini.
