TIMU ya Boda Boda FC imetwaa ubingwa wa michuano ya YAS 5G Cup Geita 2026 baada ya kuifunga timu ya SGA Security mabao 2-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa mjini Geita.
Ushindi huo umeiwezesha Boda Boda FC kutwaa ubingwa wa mashindano hayo, huku SGA Security ikikosa nafasi ya kunyanyua kombe hilo baada ya kushindwa kupata bao katika mchezo huo.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo kumalizika, Kocha wa Boda Boda FC, Katendi Peter, alisema maandalizi mazuri ya timu pamoja na umakini wa wachezaji wakati wa mchezo ndiyo sababu kubwa iliyowasaidia kupata ushindi.

Peter alisema timu yake iliingia uwanjani ikiwa na dhamira ya kuhakikisha inapata matokeo mazuri, jambo lililowasaidia kutekeleza mipango yao na hatimaye kuibuka na ushindi.
Kwa upande wake, Kampeni wa Boda Boda FC, ameshauri mashindano hayo yaendelee kufanyika katika miaka ijayo, akisema yamekuwa chachu ya kuibua na kukuza vipaji vya vijana katika soka.
Naye Msimamizi wa SGA Security Geita, Dickson Wepi, alisema timu hiyo ina kila sababu ya kukubali matokeo yaliyopatikana kutokana na namna mchezo ulivyoendeshwa kwa haki tangu ulipoanza hadi kumalizika.
Wepi alisema pamoja na kutopata ushindi, wamejifunza kutokana na mchezo huo na wataendelea kufanya maandalizi zaidi ili kufanya vizuri katika mashindano yajayo.
Naye Meneja wa YAS Mkoa wa Geita, Willington Byekwaso, alisema mashindano hayo yataendelea kufanyika na kwamba wamejipanga kuhakikisha yanawafikia wananchi waliopo katika maeneo ya pembezoni mwa Mji wa Geita.
Byekwaso alisema lengo ni kutumia michezo hiyo kuwafikia vijana wengi zaidi na kuwapa fursa ya kuonesha vipaji vyao, huku kampuni hiyo ikiendelea kushirikiana na jamii katika shughuli mbalimbali.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Polisi ambaye pia ni Polisi Jamii Mkoa wa Geita, Amina Kahando, alisema michezo imeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuwaunganisha wananchi na Jeshi la Polisi.
Kahando alisema ushirikiano huo ni muhimu katika kujenga mahusiano mazuri kati ya wananchi na Jeshi la Polisi, pamoja na kuhamasisha vijana kutumia muda wao kushiriki katika shughuli zenye manufaa kwa jamii.